Uamuzi wa kesi ya ununuzi wa wilbaro kumi waahirishwa

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - DERICK LUVEGA Na SHABAN MAKOKHA

MAHAKAMA ya Kakamega, jana iliahirisha kutoa uamuzi katika kesi ambayo watu saba wameshtakiwa kwa kuongeza bei ya wilbaro kumi zilizonunuliwa na kaunti ya Bungoma mwaka jana.

Hakimu Mkuu Bildad Ochieng alisema uamuzi huo sasa utatolewa Mei 31. Alisema hakuwa tayari kutoa uamuzi kwa sababu ya kusongwa na kazi.

Watu hao saba walifika katika mahakama ambayo ilikuwa imejaa watu wakiwa tayari kujua hatima yao lakini Bw Ochieng akasikitika na kuwafahamisha kwamba hakuwa tayari kutoa uamuzi.

“Kutokana na shinikizo za kazi, uamuzi umeahirishwa hadi Mei 31. Ninaomba radhi kwa hali hii,|” alisema. Washtakiwa walimsikiliza hakimu na kisha wakaondoka mahakamani kwa haraka baada ya uamuzi kuahirishwa.

Washtakiwa hao ni mwenyekiti wa kamati ya kutoa zabuni

Bw Howard Lukadilu, naibu wake Oscar Onyango Ojwang’ na Bw John Juma Matsanza.

Wengine ni Bw Ayub Tuvaka China, Arlington Shikuku Omushieni, Jacquiline Nanjala Namukali na Reuben Cheruiyot Rutto.

Wanakabiliwa na mashtaka ya kununua toroli kumi za kutumiwa katika kichinjio kaunti ya Bungoma.

Inadaiwa kwamba kila toroli ilinunuliwa kwa Sh109,320 kutoka kwa kampuni ya Jagla Enterprises.

Wilbaro hizo zilinunuliwa wakati wa utawala wa aliyekuwa gavana Kenneth Lusaka ambaye sasa ni spika wa seneti.

Kesi ilipokuwa ikisikilizwa, wakili wa washtakiwa Bw Sylvester Madialo alikosoa upande wa mashtaka akisema ulishindwa kuthibitisha kesi dhidi ya washtakiwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.