Rais al-sisi aachilia wafungwa 33O mwezi mtukufu wa Ramadhani ukianza

Wengi wa walioachiliwa walikamatwa kwa kuandamana kupinga utawala wake

Taifa Leo - - Habari Za Afrika Na Dunia - Na MASHIRIKA

RAIS wa Misri Abdel Fattah al-sisi Jumatano aliwaachilia huru wafungwa 330 kuadhimisha mwanzo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, wengine wakiwa na wale waliokamatwa kwa kuandamana kupinga utawala wake.

“Namwamuru Waziri wa Masuala ya Ndani kuhakikisha kuwa watu hawa wameachiliwa huru ili waungane na familia zao kwa suhur, (chakula kinachaliwa kabla ya kuanza kwa Ramadhan,” Sisi akasema kwenye mkutano wa vijana kwenye hotuba iliyopeperushwa moja kwa moja katika runinga ya kitaifa.

Wengi wa wafungwa hao ni vijana kati ya umri wa miaka 18 na 35.

Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, ambapo Waislamu hushinda mchana kutwa bila kula chakula au kunywa maji ulioanza jana.

Mnamo 2016 Rais Sisi aliahidi kuwaachilia huru vijana waliofungwa jela katika msako dhidi ya wafuasi wa aliyekuwa Rais wa Misri Mohamed Morsi ambaye aling’olewa mamlakani na wanajeshi mnamo Julai 2013.

Hii ni kufuatia msururu wa maandamano ulioendeshwa na vijana hao wakipinga mapinduzi hayo ambayo yaliongozwa na Sisi ambaye alikuwa mkuu wa majeshi.

Kuachiliwa kwa wafungwa hao 330 kunatokana na mapendekezo ya Kamati ya Msamaha wa Rais ulioundwa mnamo 2016. Hii ni kufuatia mapendekezo yaliyofikiwa katika kongamano la vijana lililoandaliwa mwishoni mwa mwezi Oktoba 2016 katika jiji la Sharm el-sheikh lililoko karibu na bahari ya Red Sea.

Ni baada ya kongamano hilo ambapo Rais Sisi aliwaachilia huru wafungwa 82, wengi wao wakiwa wanafunzi wa vyuo vikuu, mnamo Novemba 2016. Na wengine 203 waliachiliwa huru mnamo Machi 2017.

Jana, Raia wengi walichangamkia habari za kuachiliwa huru kwa wafungwa hao zilichapishwa katika magazeti makuu nchini Misri.

“Takriban vijana 332 wameachiliwa huru chini ya msamaha wa Rais huku Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ukianza leo (jana),” likaripoti

gazeti la Akhbar al-youm linalomilikiwa na serikali.

“Tunampongeza Rais Sisi kwa kuamuru kuachiliwa kwa watu hawa ambao walikamatwa kwa kutekeleza haki yao ya kuandamana kupinga udhalimu,” akasema mwanamume mmoja ambaye alibana jina lake.

Utawala wa Sisi umekuwa ukikabiliana na maasi kutoka kwa wafuasi wa Morsi waliopinga kuondolewa kwake mamlakani.

Maelfu ya wafuasi hao wametupwa gerezani baada ya kukamatwa na maafisa wa usalama tangu mwaka wa 2013.

Picha/afp

Al-sisi akihutubia wanahabari awali jijini Cairo. Ameachilia wafungwa 330 kuadhimisha mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.