Tulipofika Ufisadi ni janga la kitaifa

Taifa Leo - - Barua -

UMEFIKA wakati ambapo Ufisadi unafaa kutangazwa rasmi kuwa janga la kitaifa. Haiyumkiniki kwamba taifa linaweza kupoteza Sh10 bilioni kupitia kwa ufisadi kisha mambo yaendelee tu kana kwamba hakuna kilichofanyika.

Kuibuka kwa kashfa nyingine katika Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) ambapo inadaiwa kwamba Sh10b ziliporwa ni jambo ambalo limeatua mioyo ya watu wengi.

Miaka kadhaa iliyopita NYS ilipopoteza zaidi ya Sh720 milioni, Wakenya, asasi kama vile ya ujasusi, Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi nchini pamoja na Kiongozi Mkuu wa Mashtaka pamoja na kamati ya Bunge kuhusiana na Matumizi ya Pesa za Umma kwa pamoja ziliingilia kati suala hilo na baadhi ya maafisa washukiwa wakafikishwa mahakamani hata ingawa kufikia sasa hakuna aliyefungwa. Kwa wakati huo shinikizo lilimfanya Rais kuwasimamisha mawaziri kadhaa kazi na kufanya mageuzi kadhaa katika serikali yake.

Katika awamu hii ya pili ya uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta, kiwango kingine cha kima cha Sh10b kuripotiwa kuibwa ni jambo linaloshtua sana. Wakenya wengi hawana tumaini kwamba hatua madhubuti zitachukuliwa na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria. Hii ni kwa sababu hakuna adhabu ya mno ambayo imewahi kutolewa awali kulipotokea matukio mengine ya wizi wa pesa za umma.

Taifa la Kenya linaendelea kusalia nyuma kimaendeleo kutokana na adui wawili; ukabila na ufisadi. Serikali zote za awamu zilizopita zimefeli vibaya katika vita dhidi ya ufisadi. Taasisi zilizoundwa kukabili uozo huu wa kimaadili pia zimefeli. Hii ndiyo maana ufisadi unafaa kutangazwa janga la kitaifa.

Katika mataifa yaliyoendelea na kufaulu katika vita dhidi ya ufisadi, Rais huwa katika mstari wa mbele. Wakati umefika kwa Rais Uhuru Kenyatta kuamua kuwafurusha serikalini maafisa wanaoiba mali ya umma na mali zao ziuzwe ili kurejesha pesa walizoiba mbali na wao kufikishwa mahakamani kushtakiwa.

Ikibidi taifa linafaa lishirikishwe katika uundaji wa sheria mpya yenye makali kukabili ufisadi kwa sababu ni wazi kwamba za sasa zimeshindwa kunyaka wafisadi. Kwa mujibu wa wataalamu wa uchumi, zaidi ya nusu ya pesa ambazo hutengwa katika bajeti kwa maendeleo huwa zinapotea kupitia mianya ya ufisadi. Ama kweli bila kukabili ufisadi taifa hili lisitarajie maendeleo yoyote ya mno.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.