Alinidanganya hajaoa, sasa nimejua ana mke

Taifa Leo - - Fumbo & Falaki -

Kwako shangazi. Kuna mwanamume tuliyependana na nikaamuliza kwanza kama ameoa akaniambia hajaoa. Tulichumbiana na hatimaye tukaoana na sasa tuna mtoto mmoja. Tumekuwa tukiishi mjini na nilishtuka sana juzi mtu fulani jirani yao nyumbani aliponiambia kuwa mume wangu ana mke na watoto watatu kwao mashambani. Sasa nimechanganyikiwa, sijui nimuache ama niendelee kuishi naye. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Siku hizi watu wamekuwa waongo sana na hufai kuamini chochote tu unachoambiwa, unahitajika kupiga hatua zaidi kuthibitisha. Ulifanya makosa kukubali kuolewa na mwanaume huyo kabla hajakupeleka nyumbani kwao kukujulisha kwa wazazi na jamaa zake. Kama ungechukua hatua hiyo mapema ungejua kuwa ana mke. Uamuzi wako sasa utategemea iwapo uko tayari kuwa mke wake wa pili kwani unasema mmezaa pamoja.

Ameanza kujipalilia akisema sijui kulima

Humjambo shangazi? Nina mwanamke mpenzi wangu wa miaka miwili. Juzi nilishangaa nilipoenda nyumbani kwake nikampata akijishughulikia kwa kutumia kifaa fulani cha plastiki. Nilipomuuliza alinilaumu mimi akidai simtoshelezi. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Kuna usemi kuwa kuona ndiko kuamini. Ulimfumania peupe mwenzako akijishughulikia ili kumaliza kiu ambayo umemuachia. Sasa umejua ukweli ni wajibu wako kufanya juu chini kuhakikisha unawajibika ipasavyo chumbani ili kumuondolea mahangaiko.

Mwanamke yupi mzuri?

Shangazi kuna jambo linalonisumbua moyoni. Ni mwanamke gani kati ya hawa ambaye ni mzuri? Anayekwambia akitongozwa na wanaume wengine ama anayejinyamazia tu na kuweka jambo hilo kuwa siri?

Kupitia SMS

Wanawake ni tofauti. Kuna wanaoamini kuwa ni vizuri kuwaambia waume au wapenzi wao wakitongozwa na wanaume wengine na kuna wale wanaoamini ni vizuri kunyamaza tu. Hakuna jambo baya kati ya hayo mawili, bora tu mwanamke adumishe uaminifu wake kwa mumewe au mpenzi wake.

Aliniachia watoto sasa ni miaka tisa, anataka kurudi

Shangazi kuna jambo ninaomba unisaidie kutatua. Mimi ni baba ya watoto watatu ingawa kwa sasa hatuishi na mke wangu. Kisa ni kwamba siku moja nilienda safari ya siku mbili na niliporudi nikapata amebeba kila kitu nyumbani na kuniachia watoto. Nilipompigia simu aliniambia hatawahi kurudi kwangu. Baada ya miaka tisa ameanza kunipigia simu akisema anataka kurudi kwa watoto wake. Ukweli ni kuwa simtaki kwa sababu ya alivyonitendea. Nishauri.

Kupitia SMS

Kilichomfanya mke wako atoroke na kukuachia watoto anakijua yeye mwenyewe. Hata hivyo, ni wazi kwamba mipango aliyokuwa nayo imetibuka na sasa anajuta. Ukweli ni kwamba alikukosea na una haki ya kuchagua kumkataza kurudi kwako ama kumsamehe na kumkubali tena. Fanya uamuzi wako.

Namshuku mpenzi

Vipi shangazi. Kuna mwanaume tuliyejuana majuzi ambaye ananipenda na mimi pia nampenda. Hata hivyo nimeanza kushuku kuwa huenda ana mwingine. Juzi nilimpigia simu ikachukuliwa na mwanamke aliyedai simu hiyo ni yake. Nilipomuuliza mwanaume huyo baadaye alidai eti aliacha simu kwa gari na kulikuwa na watu wengine humo ndani. Tafadhali nishauri, naogopa kuchezewa. Kupitia SMS

Siku hizi watu walio na wapenzi wengi wanatumia mbinu nyingi kudumisha mahusiano hayo. Kuna uwezekano mkubwa kwamba mwanamke aliyepokea simu hiyo ni mpenzi wake na ndiyo sababu alipata ujasiri wa kukwambia kuwa ni yake. Ni muhimu umchunguze mwanaume huyo ujue mienendo yake vizuri kabla hujampa moyo wako.

Amesema hanipendi

Shikamoo shangazi. Nilishangaa sana juzi mwanaume mpenzi wangu alipoungama kuwa hanipendi wala hajawahi kunipenda. Aliniambia alianzisha uhusiano na mimi ili kumtia wivu mwanamke mwingine aliyemtongoza na akamkataa. Nilikuwa nimempa moyo wangu wote nikidhani alinipenda kwa dhati. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Kungekuwa na sheria ya kuwashtaki walaghai wa kimapenzi kisha niwe jaji mahakamani, ningemhukumu kifo mwanaume huyo. Ni makosa kuchezea hisia za mtu kwa madai unampenda ilhali unajua kwa hakika humpendi. Achana naye aendelee na sarakasi zake. Njia ya muongo ni fupi na malipo ni papa hapa duniani.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.