Maudhui makuu katika hadithi ‘Tumbo Lisiloshiba’

Ndiyo hadithi ya kwanza katika diwani ‘Tumo Lisiloshiba’ inayotahiniwa katika shule za sekondari humu nchini

Taifa Leo - - Jaribio La Kcse 2018 Cre 2 - akamau@ke.nationmedia.com

TUMBO Lisiloshiba’ ndiyo hadithi ya kwanza katika diwani ‘Tumo Lisiloshiba’ iliyohaririwa na waandishi Dumu Kayanda na Alifa Chokocho. Ni hadithi iliyoandikwa na Prof Said Ahmed Mohamed.

Baadhi ya maudhui makuu yanayojitokeza katika katika hadithi hii ni: Utabaka, ufisadi, ukandamizaji/udhalilishaji wa wanyonge, ubaguzi wa kiuchumi na umoja.

UTABAKA

Utabaka unadhihirika pale inadhihirika kwamba wahusika kama Mzee Mago wanaishi katika mtaa wa Madongoporomoka, ambao unarejelewa kuwa wa watu wa kipato cha chini. Katika hadithi, mtaa huo pia ndiko kulikojengwa vibanda vidogo vya kibiashara, k.m hoteli ya Mzee Mago ambayo inabomolewa na tinga linalotumwa na bwanyenye anayekula katika hoteli hiyo.

Mwandishi anaeleza: “…mji ulijaa, ambapo lazima ardhi mbadala ingetafutwa katika eneo la Madongoporomoka-kule kunakoishi wepesi wasio na mashiko, kunako mashonde ya vinyesi, kunako vibanda uchwara” (uk4).

Bali na hayo, tajiri huyo amebebwa kwa gari la kifahari aina ya Audi Q7 na dereva wake, wakati ubomoaji unaendelea. Hili ni kinyume na akina yakhe wa Madongoporomoka ambao wanaishi katika hali za kesho itakuwaje.

Ufisadi na ukandamizaji wa watu maskini

Ufisadi unajitokeza katika mchakato mzima wa jinni inagunduliwa kwamba ni ardhi ya eneo la Madongoporomoka ambapo “kutatafutwa nafasi mbadala” za ujenzi wa majumba ya tajiri yule. Hatuelezwi taratibu zinazofuatwa katika kuitambua ardhi husika. Hakuna asasi za usimamizi wa masuala ya ardhi kama Wizara ya Ardhi ama maafisa wake wanaohusishwa, ila kile tunachoona ni bwanyenye anayejitokeza na kudai kwamba Wanamadongoporomoka watambue kwamba “ardhi hiyo si yao.”

Linalofuata ni uwepo wa matinga ambayo yanabomoa vibanda vya Wanamadongoporomoka, bila kuzingatia vigezo vya kisheria ambavyo huwa msingi wowote wa utekelezaji wa ubomozi.

Zaidi ya hayo, ubomozi huo ni ishara ya ukandamizaji wa watu maskini wa Wanamadongoporomoka. Sababu kuu ya hili ni kwamba kabla ya kutekelezwa kwa ubomozi huo, bwanyenye huyo anatoa vitisho kwa Mzee Mago na wenzake kwamba hawatakuwa na usemi wowote ubomozi huo utakaotelelezwa.

Jitu hilo linamwambia Mzee Mago: “Nitakusaidia vipi”? Nitakula chakula chako chote ulichopika kuwauzia wateja wako leo,”(uk 8). Hii ni ishara ya vitisho na ukandamizaji wa watu maskini.

Ubaguzi wa kiuchumi

Taswira inayojitokeza katika hadithi hii ni mgawiko wa maeneo mawili ambayo yamegawanyika pakubwa kwa misingi ya kimapato na uwepo wa huduma muhimu ambazo zinatolewa na serikali.

Kwa mfano, eneo moja la jiji linarejelewa kuwa lenye uwezo mkubwa wa kiuchumi, na lililostawi sana kimaendeleo.

Inaelezwa: “jili lenyewe lilipiga muhuri wa kujitambulisha kwa upeo wa nafasi, usafi na ujumi na tamaduni mchanganyiko: hoteli, mikahawa, majumba ya muziki, maduka kuu, departmental stores, casinos…” (uk4).

Aidha, hilo linaonyesha umuhimu mkubwa wa kiuchumi ulio katika mji huo; na mikakati ambayo utawala husika unachukua ili kupanua nafasi ya ujenzi wa majengo zaidi ya kuimarisha uchumi. Jawabu hili linapatikana katika kubomoa vibanda vya Wanamadongoporomoka bila kufuata taratibu zifaazon za kisheria.

Na kinyume na mji huo, mtaa wa Madongoporomoka unatajwa kuwa duni kwa maisha ya binadamu: “ …bubujiko la maji machafu. Kunako makaro na uvundo unaopasua mianzi ya pua. Kunako pachapacha za kila kitu..”(uk4).

Hii ni ishara kwamba utawala uliohusika haujali maslahi ya wakazi wa eneo hili, licha ya hatari za kiafya zilizo katika mazingira wanamoishi.

Umoja, ushujaa na utetezi wa haki

Licha ya changamoto na ukandamizi huu wote, upekee mkuu unaojitokeza ni umoja unaodhihirishwa na Wanamadongoporomoka. Wanaibukia kuwa watu wanaojaliana hali, kiasi cha kutotishika na njama za kuwabomolea vibanda vyao.

Kwa mfano, Mzee Mago anajitokeza kusumbuliwa sana na juhudi za watu matajiri kutaka kunyakua ardhi za maskini.

Hili linamfanya kuwakutanisha wenzake ili kujadilia hilo (uk 2). Juhudi zake zinawafanya wakazi hao kugundua mapema njama hizo, hali ambayo inawapa motisha kuimarisha zaidi umoja miongoni mwao.

Baadhi ya wale ambao wanaojitokeza kiwazi kuapa kukabili njama hizo ni Bw Kabwe na Bi Fambo, ambao wanatoa kauli ya kutetea haki zao kwa njia zozote.

Ni hali inayodhihirika kwani hata ya vibanda kubomolewa, wanaapa kutoondoka katika ardhi hiyo kwa kuvijenga upya.

WANDERI KAMAU “Hii ni ishara kwamba utawala uliohusika haujali maslahi ya wakazi”

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.