Mwenyezi Mungu humimina rehma zake kwa waja katika kumi la kwanza

Taifa Leo - - Mawaidha Ya Kiislamu - Na ALI HASSAN Ijumaa Karim

Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo. Tumejaaliwa siku nyingine hii tukufu katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan ili tuweze kuambizana mawili matatu kuihusu dini yetu tukufu ya Kiislamu.

Awali ya yote kama ilivyo dini yetu tukufu ya Kiislamu ni kukumbushana kuwa hapana mwingine anayepaswa kuabudiwa kwa haki ela Mola wetu mmoja pekee: Allah (SWT). Kwa maana hiyo ni kuwa hapana mwingine anayepaswa kuabudiwa kwa haki ela yeye yuyo huyo Muumba wetu mmoja, mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo.

Na ni yeye pekee anayestahili heshima na shukrani na kuabudiwa kwa kuwa ndiye pekee aliyeumba ardhi na mbingu na vyote vilivyomo, kwa maana ya viumbe vyote. Hivyo basi ni yeye pekee mwenye uwezo wa kuumba na kuumbua.

Katika uzi uo huo twachukua nafasi hii kumtilia dua na kuzidi kuitakia aila yake kila la kheri mwombezi wetu, bwana wetu, Mtume (SAW).

Raha iliyoje ndugu yangu kukutana leo hii katika funga hii ya mwezi mtukufu wa Ramadhan. Yaani ni kwa vipi miye na wewe ndugu yangu yafaa kumshukuru Mola wetu kwa kutujaalia kuufikia mwezi huu wa toba, mojawapo wa nguzo kuu tano zadini hii tukufu ya Kiislamu.

Mwezi ambao mbali na thawabu za kila aina, pia ni mwezi wenye mengi ya kusemwa! Ni mwezi ambao umegawiki katika makundi matatu makuu ambayo ni maarufu kama makumi matatu. Kila kumi na mgawo wake.

Kwa sasa tujikite kidogo katika kumi hili la kwanza. Kumi la kwanza linajulikana kwa jina la Rehma (rehema). Katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani vitu vinavyopaswa kufanywa zaidi ni kuswali, kutoa zaka na matendo mengine ambayo kwa kiasi kikubwa humpwekesha Mwenyezi Mungu.

Katika mwezi huu, kila jema analofanya mja hulipwa zaidi kuliko ambavyo analipwa katika siku za kawaida, ndiyo maana watu hufurika kwa wingi katika nyumba za ibada. Kumi la Rehma hupata baraka na kwa kila anachokifanya huku shetani akifungwa minyororo ili asiweze kuwarubuni watu.

Kwa mujibu wa vitabu mbalimbali vya dini Malaika hushuka ardhini kutafuta watu wenye kusoma Qur-an au kufanya ibada mbalimbali ambazo humpwekesha Mwenyezi Mungu.

Mja yeyote ambaye Malaika wakimkuta akifanya ibada na kusoma Qur-an, huwa mwenye kupata daraja ya juu kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kufunguliwa mambo yake mengi ambayo yalikuwa yamekwazika.

Kwa kifupi ni kuwa huu ni mwezi wa kuvuna na hivyo basi twamwomba Mumba wetu atujaalie tuyajaze makapu kwa makapu ya thawabu. Na kuchuma huko kumeanza tayari katika kumi hili la kwanza.

Mwezi huu ni wa mchumo kwa mja, kwa kuwa kila jambo jema analolifanya hulipwa maradufu (thawabu) na kwa mwenye kufanya maasi hakika atakuwa ni mtu mwenye kula hasara mbele ya Mungu na anakabiliwa na adhabu kubwa siku ya kiama.

Mwezi huu ni kama chuo cha mafunzo ambapo baada ya kumalizika, waumini wanapaswa wawe wameelimika na kubadilika ili wawe kama wamezaliwa upya kutokana na kutakasika na maovu.

Haitarajiwi hata kidogo kwa ambaye amejinyima kula (amefunga), kufanya ibada, kusoma Qur-an na mambo mengine mema, kuanza kufanya maasi mara baada ya kumalizika kwa mwezi huu.

Imekuwa desturi kwa baadhi ya Waislamu kuuthamini na kuuona mwezi mtukufu wa Ramadhani ndiyo pekee wa kumuabudu Mwenyezi Mungu na kufanya amali njema huku wakiiona miezi mingine kama wamehalalishiwa kufanya maasi. Dhana hii inapaswa kuachwa kwa kuwa haitakuwa na maana kama muumini aliyepita katika chuo cha mafunzo (Ramadhani) akalingana au kumzidi yule asiyepitia katika chuo hicho.

Mwenye kurejea kufanya maasi mara baada ya Ramadhani, atakuwa ni sawa na mtu aliyejisafisha vizuri na kuvaa nguo nyeupe, kisha akajirusha kwenye matope.

Misingi ya Kiislamu, nayo hujengwa na nguzo kuu tano ambazo kwanza ni kushuhudia kuwa na imani kuwa hapana Mola anayepaswa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu mmoja na kwamba Mtume Muhammad (SAW) ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu.

Nguzo ya pili ni kusimamisha swala tano kwa maana ya kudumu kutekeleza ibada hiyo, yaani Alfajiri, Adhuhuri, Alasiri, Magharibi na Isha, na ya tatu ni kutoa zaka kwa wenye uwezo.

Mihimili mingine miwili ya Uislamu baada ya Shahada, Swala na Zaka ni kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, nguzo ambayo ndiyo kiini cha makala hii.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.