SHINDANO LA UANDISHI WA INSHA

Licha ya kung’aa katika ufunguzi mara hii walizidiwa maarifa

Taifa Leo - - Front Page - GEOFFREY ANENE NA JOHN KIMWERE

MALKIA Strikers ya Kenya ilikosa majibu kwa mashambulizi makali ya Serbia na kukung’utwa kwa seti 3-0 katika mechi yake ya pili kwenye mashindano ya dunia ya voliboli ya wanawake mjini Hamamatsu, Japan, jana.

Vipusa wa kocha Japheth Munala, ambao walishangaza Kazakhstan 3-0 katika mechi yao ya ufunguzi, walizidiwa maarifa katika kupenyeza ukuta wa Serbia uliozima makombora mengi.

Nahodha Mercy Moim aliendelea kuongoza ufungaji wa pointi wa Kenya akipata nane dhidi ya Serbia. Jovana Stevanovic, Brankica Mihajlovic na Stefana Veljkovic waliongoza kufungia Serbia alama baada ya kupachika alama tisa, nane na saba, mtawalia. Seti ya kwanza ilishuhudia Kenya na Serbia zikipoteza alama kwa urahisi kwa kupiga mipira mirefu iliyotoka nje ama kupiga neti zilipokuwa zikianzisha mpira.

Baada ya kushinda seti ya kwanza, mchezo ulikubali Serbia, ambayo iliaibisha Kenya katika seti mbili zilizofuata kwa kuishinda 25-9 na

25-8, mtawalia. Serbia, ambayo ilipapura Jamhuri ya Dominican 3-0 katika mechi ya ufunguzi, inaongoza Kundi D kwa alama sita. Inafuatiwa na Brazil, ambayo pia ilizaba Puerto Rico na Dominican kwa seti za kufanana 3-0.

Puerto Rico, ambayo pia ililemea Kazakhstan 3-0, imerukia nafasi ya tatu na kusukuma Kenya katika nafasi ya nne kwa tofauti ya ukubwa wa kichapo. Zote mbili zimezoa alama tatu kila mmoja. Kazakhstan na Dominican zinashikilia nafasi mbili za mwisho bila alama kutokana na vichapo viwili mfululizo. Bara Afrika ilikuwa na siku mbaya jana. Baada ya kuanza kampeni kwa kucharaza Mexico 3-1 katika mechi ya Kundi A , mabingwa wa Afrika Cameroon walitandikwa 3-0 na Ujerumani.

Kenya itakuwa na mtihani mgumu dhidi ya Puerto Rico leo. Kikosi cha Malkia Stars: Trizah Atuka, Edith Wisa, Lorine Chebet, Christine Siwa, Mercy Moim, Noel Murambi, Jane Wacu, Janet Wanja, Violet Makuto, Emmaculate Chemtai, Elizabeth Wanyama, Aggripina Kundu, Sharon Chepchumba na Leonida Kasaya.

Picha/afp

Kikosi cha Taifa cha Kenya cha mchezo wa voliboli almaarufu Malkia Strikers kikisherehekea baada ya kuikalifisha Kazakhstan katika mchuano wa ufunguzi juzi. Jana vipusa hawa walisakamwa na Serbia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.