Wakazi wazidi kuteseka huku Wairia na kampuni wakizozana

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - Na NDUNG’U GACHANE

WAKAZI wa Kaunti ya Murang’a wanazidi kuteseka kutokana na mvutano uliopo kati ya serikali ya kaunti na kampuni za kusambaza maji kuhusu ulipaji madeni yao.

Gavana Mwangi wa Iria ametoa agizo kwa wakazi kutolipa madeni yao hadi pale serikali yake itatangaza akaunti mpya. Kwa upande mwingine, kampuni za maji zimeendelea kuwakatia maji wale ambao wamekosa kulipa fedha hizo.

Akieleza sababu za kutoa maagizo hayo, Bw Wa Iria alisema kuwa hajazipa kibali kampuni hizo kukusanya pesa kutoka kwa wananchi kwa niaba ya serikali yake.

Alisema serikali ya kaunti inajitayarisha kubuni akaunti mpya ambapo fedha zote zitakazokusanywa zitawekwa.

Mmoja wa waathiriwa hao ni Bw Martin Mwaura aliyesema kuwa maji yake yalikatwa baada yake kutolipa Sh4, 200 kwa Kampuni ya Kusambaza Maji ya Murang’a (MUWASCO). Kulingana na Bw Mwaura, huwa analipa Sh1,500 kila mwezi, ila alishangazwa na deni lake kufikia Sh4, 200. Licha ya hayo, kampuni hiyo imesisitiza kwamba lazima alipe pesa hizo ili aweze kurejeshewa maji.

Alisema kuwa alitafuta usaidizi kutoka serikali ya kaunti kutokana na agizo la gavana kwa mafundi wa mifereji kuwaunganishia maji tena. Licha ya hayo, kampuni hiyo ilimwondolea mita ya mifereji kadhaa, ila mara hii ikamwagiza kulipa Sh707 badala ya Sh4,200.

Hata hivyo, kampuni inashikilia kwamba ni watu wachache sana ambao wanazingatia maagizo ya Bw Wa Iria kwa kuwa asilimia 82 ya wateja wao wamelipa ada zao zote.

“Idadi kubwa ya wateja wetu wamelipa ada zao kikamilifu, hivyo hawajaathiriwa kwa vyovyote na maagizo ya gavana,” akasema Mhandisi Daniel Ng’ang’a.

Mzozo huo umekuwa mbaya zaidi kutokana na misimamo mikali ya pande zote husika.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.