Bilbao Queens wanalenga kuwania ubingwa Ligi Kuu

Taifa Leo - - Gumzo La Spoti - NA IGNATIUS OUNDO

KATIKA miaka ya hapo nyuma, soka ya kinadada nchini ilikuwa ikupuuzwa na wengi kinyume na kabumbu ya wanaume.

Wengi walijaa dhana potovu kwamba, wasichana hawana uwezo wa kutandaza kandanda tamu jinsi walivyo wanasoka wa kiume. Kupuuzwa huko kulichangia wasichana wengi kujiingiza kwenye vitendo vichafu bila kujali maisha yao ya usoni.

Hata hivyo, dhana hiyo inaonekana kuzikwa kwenye kaburi la sahau baada ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kufanyiwa marekebisho. Tangu marekibisho hayo yafanyike miaka michache iliyopita, tumeshuhudia klabu nyingi za kina dada zikiundwa katika maeneo tofauti nchini kwa dhamira ya kuwapa vipusa fursa ya kuonesha vipaji vyao.

Bilbao Queens ni moja kati ya klabu za wasichana zilizobuniwa miaka miwili iliyopita kwa madhumuni ya kuinua mchezo wa soka miongoni mwa wasichana. Klabu hii kutoka eneo la Kayole Mashariki, Nairobi imeanza kuonesha dalili za kufika mbali kisoka.

Chini ya kocha Vincent Oduor, Bilbao Queens wamezama kwenye mazoezi ya kufa-mtu katika jitihada za kunoa makali yao huku wakilenga kufikia klabu za hadhi kama vile Oserian Ladies, Kisumu All Stars, Vihiga Queens, Mathare United Woman na Eldoret Falcons ambazo zinatia fora kwenye Ligi Kuu ya wanawake hapa Kenya.

"Kufunza wasichana soka ni kazi ngumu sana inayohitaji moyo wa kujitolea na kujiamini. Licha changomoto hiyo, huwa nahakikisha wasichana hawa wanachapa mazoezi ya kufana kwa ajili ya kuboresha mchezo wao," asema kocha.

Kulingana na kocha huyo, baada ya kufanya mazoezi pamoja na kucheza mechi nyingi za kupimana nguvu kwa zaidi ya mwaka mmoja, klabu hii iliamua kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha Aids Awareness Cup na bila shaka iliibuka bingwa wa hata licha ya kuwa mara yao ya kwanza kushiriki mechi za kuwania mataji.

Kocha Oduor aliunda kikosi thabiti kilichojumuisha wachezaji wenye ujuzi ajabu wa kucheza soka kama vile Ann Wangui na Mary Wahu kwa ajili ya kutwaa ubingwa wa Kombe hilo lililoandaliwa na Hospitali ya Patanishao.

Bilbao Queens ilihifadhi ubingwa huo baada ya kutatiza wapinzani Tumaini FC na hatimaye ikawazaba mabao mabao 2-1 kwenye mechi ya fainali iliyofanyika uwanjani Jacaranda mwezi jana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.