Omog, Mkude ni vita; Kapombe safii

Bingwa - - HABARI - ZAINAB IDDY NA MARTIN MAZUGWA

KUONYESHA kuwa hataki masihara katika michezo ijayo ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara ili kutimiza lengo lao la kutwaa ubingwa msimu huu, Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, ameanza kuwashughulikia nyota wake wanaoonekana kumkwaza katika kutimiza azma yake hiyo.

Hilo limejitokeza katika mazoezi yaliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, baada ya nahodha wa zamani wa kikosi hicho, Jonas Mkude, kukumbana na adhabu ya kocha huyo kutokana na kuchelewa kuwasili mazoezini.

Katika mazoezi hayo, Mkude aliwasili uwanjani hapo saa 09:48, ikiwa ni robo saa baada ya wenzake kuanza mazoezi wakiwa tayari yameshafanya yale ya kupiga pasi, kukokota mpira pamoja na mazoezi ya kupiga vichwa yaliyokuwa yakiongozwa na kocha msaidizi, Jackson Mayanja.

Mara baada ya kujiandaa na kuingia uwanjani, Mkude alikwenda moja kwa moja kwa Omog, ambaye alimtaka nyota huyo kuzunguka nusu uwanja, huku kocha huyo akiangalia muda.

Mkude alitumia dakika 15 kufanya adhabu aliyopewa na kocha wake, akiwa amezunguka nusu uwanja mara saba kabla ya kuruhusiwa kujiunga na wenzake kwa ajili ya programu nyingine.

Katika hatua nyingine, Mayanja amelithibitishia BINGWA kuwa, beki wao kiraka, Shomari Kapombe, anatarajia kuanza rasmi mazoezi baada ya mchezo dhidi ya Mwadui, utakaochezwa Jumapili, kwenye Uwanja wa Uhuru.

Kapombe, anayesumbuliwa na majeraha ya nyonga, aliyoyapata alipokuwa akikitumikia kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars, amekosa michezo mitatu ya timu yake hiyo, akianzia na ule wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na michezo miwili ya Ligi Kuu Bara, dhidi ya Ruvu Shooting na Azam.

“Kapombe anatarajia kuungana na wenzake baada ya kukaa nje ya kikosi kwa muda mrefu tangu alipojiunga na Simba, kwa upande wa Paul Bukaba, ameelekea nchini Burundi kufuata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) katika timu yake,” alisema Mayanja.

Mkude

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.