Simba wapita njia za Yanga

Bingwa - - HABARI - ZAINAB IDDY NA MARTIN MAZUGWA

KATIKA kuonyesha jinsi Simba ilivyopania kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, benchi la ufundi la timu hiyo limeamua kufanyia kazi suala zima la umakini kwa wachezaji wao kuhakikisha hawafanyi kosa lolote wawapo uwanjani.

Wiki iliyopita, Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, alitumia muda mwingi wa mazoezi yake kuhimiza umakini kwa wachezaji wake, ili kuepuka kufanya makosa ambayo yanaweza kuwagharimu, lakini pia washambuliaji kutumia kila nafasi wanayoweza kuipata ya kufunga bao.

Kumekuwa na ukosefu wa umakini kwa wachezaji wengi wa hapa nchini kiasi cha kujikuta wakikosa nafasi za wazi za mabao, lakini pia mabeki wakifanya makosa yanayowagharimu na kushindwa kupata ushindi.

Bechi la ufundi la Simba chini ya Kocha Mkuu Joseph Omog, jana waliamua kulivalia njuga suala la kukosa umakini kwa wachezaji wao baada ya kutoa dozi nene katika mazoezi yaliyofanyika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Katika mazoezi hayo, Omog na msaidizi wake, Jackson Mayanja, waliwafungia kazi wachezaji wao; kuanzia mabeki, viungo na washambuliaji, kuhakikisha hawafanyi makosa, lakini pia wanatumia kila kosa litakalofanywa na timu watakayokutana nayo.

Na kwa kuwa mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Bara utakuwa ni dhidi ya Mwadui FC ya mjini Shinyanga, ni wazi kuwa wapinzani wao hao watakiona cha moto iwapo hawatajipanga.

Unajua Omog alitumia njia zipi kuwafundisha wachezaji wake umakini? Ni hivi, kocha huyo alichukua jukumu la kupanga koni zake kulingana na rangi ambapo kulikuwa na bluu na kijani, huku akiwaita wachezaji wanne wanne na kuwataka kukimbia kama wanapasha misuli, kisha kutaja rangi ya koni ili waende upande zilipo.

Ingawa Omog hakutaka kufafanua sababu za kufanya hivyo juu ya nini lilikuwa lengo lake, lakini ilionyesha wazi alikuwa akiwatengeneza katika suala zima la umakini wawapo uwanjani.

Awali, zoezi hilo lilionekana rahisi kwa wachezaji, lakini kadri muda ulivyokuwa ukienda, baadhi yao walionekana kuchemka, akiwamo winga, Shiza Kichuya.

Mchezo wa Jumapili utakuwa ni wa tatu kwa Simba wa Ligi Kuu Bara, ikiwa ni baada ya kuzivaa Ruvu Shooting waliyoichapa mabao 7-0, kabla ya kupata suluhu dhidi ya Azam FC Jumamosi iliyopita.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.