Niyonzima awatia presha mashabiki Msimbazi

Bingwa - - HABARI /TANGAZO - ZAITUNI KIBWANA NA HUSSEIN OMARY

KITENDO cha Haruna Niyonzima kukosekana kwenye mazoezi ya Simba yaliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, kimewatia presha mashabiki wa timu hiyo.

Simba inajiwinda na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mwadui FC utakaochezwa kwenye uwanja huo Jumapili, lakini Niyonzima hakushiriki maandalizi hayo kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya tumbo yaliyomuanza juzi na kupewa mapumziko ya siku mbili.

Mashabiki waliofika kwenye uwanja huo wa Uhuru walishangaa kutomwona Niyonzima, lakini daktari wa timu hiyo, Yassin Gembe, aliliambia BINGWA kuwa Niyonzima ameshindwa kujumuika na wenzake kwenye mazoezi hayo kutokana na kusumbuliwa na tumbo.

“Nilimpa mapumziko ya siku mbili kutokana na kusumbuliwa na tumbo, lakini kesho (leo) atajumuika na wenzake kama kawaida. Mashabiki wasiwe na wasiwasi,” alisema Gembe.

Gembe alisema mlinda mlango, Said Mohammed ‘Ndunda’, anaendelea vizuri, huku beki wa kulia, Shomari Kapombe, alianza mazoezi mepesi jana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.