YANGA YATUA SONGEA NA DOZI MKONONI

Bingwa - - MBELE - NA OMESMO KAPINGA

YANGA wametua mkoani Ruvuma kucheza na wenyeji Majimaji wakiwa na dozi mkononi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Majimaji

YANGA wametua mkoani Ruvuma kucheza na wenyeji Majimaji, wakiwa na dozi mkononi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Majimaji, mjini Songea.

Kikosi cha Yanga kilikuwa kimeweka kambi ya siku tatu mjini Njombe katika Hoteli ya Day To Day, kiliondoka jana kwenda mkoani humo kikiwa na matumaini ya kuibuka na ushindi mnono dhidi ya Majimaji.

Yanga, ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo, wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Njombe Mji, walioupata katika mchezo uliochezwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Sabasaba.

Ushindi huo unaonekana kuipa jeuri Yanga, lakini pia mazoezi ya nguvu waliyofanya wakiwa Njombe kabla ya kwenda kuwavaa wapinzani wao, Majimaji.

Akizungumza na BINGWA, Kocha msaidizi wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa, alisema ushindi dhidi ya Njombe Mji ulikuwa ni mwanzo wa maandalizi mengine ya kuiua Majimaji.

Nsajigwa alisema malengo yao ni kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu nyingine, kwani wamefanya maboresha katika kikosi chao kutokana na upungufu uliojitokeza mchezo uliopita.

Yanga walionekana kuanza msimu mpya vibaya, baada ya kufungwa kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 5-4, katika mchezo wa Ngao ya Jamii, baada ya kutoka sare ya kutofungana ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Baadaye walitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Lipuli, katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu Bara, uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, kabla ya kusahihisha makosa yao na kuibuka na ushindi katika mchezo uliofuata dhidi ya Njombe Mji.

Iwapo Yanga watashinda mchezo wao huo dhidi ya Majimaji, watakuwa wamefikisha pointi saba na hivyo kujiweka katika mazingira mazuri ya kuendeleza umwamba wao kwenye soka la Tanzania kwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa msimu wa nne mfululizo.

Ni mwaka wa sita sasa Yanga imekuwa ndani ya timu mbili za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na hivyo kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

JJUUKO TSHABALALA

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.