TUMUACHE RONALDO NA UEFA YAKE

Bingwa - - MBELE -

BAADA ya mafanikio makubwa Ligue 1, tajiri wa klabu ya PSG, Nasser Al-Khelaifi, ameonyesha kiu yake ya kulitaka taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, hasa kwa kitendo chake cha kumwaga mpunga mrefu kwenye soko la usajili kuwachukua Neymar na Kylian Mbappe.

Jumanne ya wiki hii, vijana wake walianza vizuri safari yao ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuichapa Celtic mabao 5-0.

Mabao ya wababe hao wa Ufaransa yaliwekwa kimiani na mastaa Mbappe na Neymar, Edinson Cavani aliyepachika mawili na Mikael Lusting.

Baada ya mchezo huo waliokuwa ugenini, wachambuzi wa soka wameanza kuamini PSG inaweza kubeba taji hilo la Ligi ya Mabingwa. Licha ya uwepo wa vigogo Real Madrid, Bayern Munich na Barcelona, hizi ni sababu zinazoweza kulipeleka taji la Ulaya nchini Ufaransa.

Ligue 1 haiwasumbui

Ligue 1 si ligi ngumu kama zilivyo La Liga, England, Bundesliga na Serie A. Wanapomaliza mechi ngumu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, PSG hawaumizi kichwa kukabiliana na timu za Ligue 1. Mfano; katika mechi zao tano tu za msimu huu, tayari wameshafunga mabao 19 na kuruhusu matatu.

Ni wazi kocha atakuwa na wakati mzuri wa kupumzisha baadhi ya nyota wake katika mechi za Ligue 1 kujiandaa na kivumbi cha Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kikosi kipana

Msimu uliopita, siri ya mafanikio ya Real Madrid ilikuwa ni kuwa na wachezaji wengi wanaoweza kukisaidia kikosi cha kwanza.

Tayari safu ya ushambuliaji ya PSG ina Neymar, Edinson Cavani, Kylian Mbappe, Julian Draxler, Angel Di Maria na Lucas.

Mbali na washambuliaji hao, safu ya kiungo ina Hatem Ben Arfa, mkongwe Javier Pastore na kinda Giovani Lo Celso, Marco Verratti, Adrien Rabiot, Thiago Motta na Christopher Nkunku.

Pembeni kuna Dani Alves, Thomas Meunier, Laywin Kurazawa na Yuri Berchiche, huku eneo la beki wa kati likiwa na mastaa watatu; Thiago Silva, Marquinhos na Presnel Kimpembe.

Neymar, Mbappe, Cavani

Neymar amekuwa kwenye ubora aliokuwa nao Santos, uliomfanya kusajiliwa na Barcelona. Wachambuzi wanaamini anataka kuthibitisha ubora wake Ligi ya Mabingwa Ulaya, akiamini michuano hiyo itakuwa safari yake ya kutwaa Tuzo ya Balon d'Or.

Dhidi ya Celtic, mbali na kufunga, Mbrazil huyo alitoa asisti ya bao la Mbappe, ambaye naye aliweka rekodi ya kuwa mfungaji mwenye umri mdogo kuzifungia timu mbili (Monaco na PSG) katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mkali Cavani alifunga mabao mawili na kuwa mchezaji wa PSG mwenye mabao mengi Ligi ya Mabingwa Ulaya. Nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay amefikisha mabao 21 na kumpiku Zlatan Ibrahimovic, aliyekuwa akiishikilia rekodi hiyo kwa mabao yake 20.

Ijumaa Septemba 8, 2017

Neymar, Mbappe na Cavan

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.