IMANI IMEMPONYA MWENDAWAZIMU FELLAINI MAN UNITED

Bingwa - - MBELE -

MCHAWI mpe mwana akulelee. Unadhani huu msemo umekosewa? Hapana, kila jambo hutokea kwa makusudi katika uso huu wa dunia, ambayo ina kiza na nuru, huku ndani yake kukiwa na mambo yanatokea.

Waangalie mashabiki wa Manchester United wanavyomtazama Maroune Fellaini ‘Big Fella’ sasa. Kila mmoja uso wake umejaa tabasamu la unafiki, huku ndimi zao zikimtaja mchezaji huyo kama shujaa wao.

Naamini ipo siku Fellaini atawarudishia mashabiki wa Manchester United sura zao za asili. Yaani ipo siku ambayo kila shabiki atamsema mchezaji huyo kwa ubaya na kusahau mazuri ambayo anayafanya.

Fellaini anavaa jezi ya Manchester United mwaka wa nne huu. Miaka minne michungu kwake, amezomewa sana, amedhihakiwa sana, kila kilicho kibaya alionekana mfano. Hakuwa mchezaji mzuri kwa kila shabiki wa United.

Binafsi sikumbuki lini alicheza vibaya zaidi ya ule mchezo dhidi ya timu yake ya zamani, Everton, kwenye Uwanja wa Goodison Park, kwa kusababisha penati dakika za usiku kabisa iliyowafanya Everton wapate pointi moja kwenye mchezo huo.

Mitandao ya kijamii ilijaa picha zake zilizoambatana na matusi, huku wengine wakimtishia kifo. Kwa ukarimu kabisa aliomba msamaha kupitia mitandao yake ya kijamii, lakini bado mashabiki walikuwa juu kutokana na hasira.

Maisha yanaenda kasi sana, Fellaini ni shujaa sasa, kila shabiki amekuwa akitabasamu anapomuona mchezaji huyo akiwa ndani ya uwanja.

Imani ya Jose Mourinho imemponya Fellaini. Amekuwa mchezaji tofauti kabisa na alivyokuwa awali. Ametulia, anakaba vizuri, na anafunga magoli muhimu kwa timu.

Maswali ni mengi kuhusu Fellaini wa sasa, je, ni mchezaji anayestahili kuchezea Manchester United? Hakika si mchezaji ambaye anaruhusiwa kusogelea jezi ya timu hiyo.

Fellaini si mchezaji mkubwa, ila ni mchezaji mwaminifu ambaye anapambana kwa ajili ya timu. Unadhani wachezaji wa aina hiyo hawakuwahi kupita pale Old Trafford? Itakuwa unajidanganya, wapo wengi tu wamepita ambao wanajulikana kama wafia timu.

John O’shea, Darren Fletcher, Wes Brown, Tom Cleverley na wengine wengi ni wachezaji ambao walikuwa wakivaa uzi wa United, lakini imani ya Sir Alex Ferguson iliwafanya waonekane wachezaji wakubwa.

Fellaini ni mchezaji muhimu sana kwenye kikosi cha sasa cha United, sababu ni mchezaji anayempa Mourinho machaguo mengi pindi anapokuwepo.

Msimu uliopita alikuwa mmoja wa wachezaji waliokuwa wakianza karibu kila mchezo kutokana na eneo la kiungo cha United kukosa mchezaji mkorofi ambaye anaweza kutibua mipango ya wapinzani.

Msimu huu tangu uanze amekuwa mchezaji anayempa Mourinho mbinu mbadala pindi timu hiyo inapohitaji matokeo. Iwe kwa kumsogeza mbele au kumuweka katikati ya dimba, Fellaini amekuwa mchezaji makini, huku akilipa fadhila za kocha huyo kwa kujituma.

“Huwa najihisi mnyonge bila Fellaini”. Alinukuliwa Mourinho baada ya Manchester United kutoa sare ya 2-2 na Stoke City. Angalia jinsi Mourinho anavyompa matumaini Mbelgiji huyo.

Kwa kawaida tumemzoea Mourinho jinsi anavyowasifu wachezaji wake ili aweze kupata ubora wao. Hicho ndicho anakifanya kwa Fellaini, na kila lililo jema linaonekana kutoka kwa mchezaji huyo.

Imani hiyo ya Mourinho imeshinda uaminifu wa Fellaini, huku kwa ujumla ikiwa kuimarika kwa kiwango cha mchezaji huyo kila siku.

Wakati yupo Everton mara nyingi alikuwa akicheza kwenye eneo la mwisho la tatu la uwanja ‘final third’, uwepo wake uliwapa wakati mgumu mabeki wa timu pinzani.

“Fellaini amekuwa mchezaji anayevutia sasa, lakini napenda Mourinho amtumie kama mshambuliaji sambamba na Romelu Lukaku, eneo hilo ndilo analolimudu vyema,” alisema Steven Gerrard wakati anafanya uchambuzi.

Fellaini si mchezaji anayenyumbulika, kucheza eneo la kiungo si nzuri sana kwake, sababu ya urefu wake na uwezo hafifu wa kumiliki mpira.

Mechi karibu zote msimu huu amekuwa nguzo muhimu, huku akitumika zaidi kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji. Ana nguvu, pia uwezo wa kupambana na mabeki kwa urefu wake.

“Si mchezaji anayeweza kufikia uwezo wa Paul Scholes, Bryan Robson au Roy Keane. Fellaini ni Fellaini, mchezaji wa pekee ambaye kila kocha anampenda kutokana na kushika maelekezo vizuri,” alisema Ryan Giggs, akimzungumzia Fellaini.

“Mara nyingi huwa anacheza kutokana na maelekezo anayoyapata, anavutia sana, kitu pekee kwake anaweza kuzalisha bao huku akisukumana na mabeki wa timu pinzani,” aliongeza Giggs.

Jaribu kukumbuka jinsi mashabiki wa Manchester United walivyobashiri kuuzwa kwa Fellaini wakati Mourinho amepewa timu hiyo. Ilikuwa tofauti, ndiye mchezaji kipenzi cha kocha huyo Mreno.

Kabla dirisha la usajili halijafungwa hivi karibuni, zilizagaa tetesi za Fellaini kujiunga na Galatasaray, lakini kauli ya Mourinho ilitosha kuzima tetesi hiyo ya mchezaji huyo kuondoka.

“Ni rahisi kunisajili mimi kuliko kumpata Fellaini. Ni mchezaji muhimu kwangu na timu pia,” alisema Mourinho.

Hamna jinsi, mwendawazimu Fellaini ameponywa na imani ya Mourinho. Lakini bado mwili wake upo nusu malaika, nusu shetani, muda wowote anaweza kukufurahisha au kukukera.

“Si mchezaji anayeweza kufikia uwezo wa Paul Scholes, Bryan Robson au Roy Keane. Fellaini ni Fellaini, mchezaji wa pekee ambaye kila kocha anampenda kutokana na kushika maelekezo vizuri,” alisema Ryan Giggs, akimzungumzia Fellaini. Imani ya Jose Mourinho imemponya Fellaini. Amekuwa mchezaji tofauti kabisa na alivyokuwa awali.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.