JJUUKO, TSHABALALA KUNA KITU

Bingwa - - MBELE - NA HUSSEIN OMAR

KUNA kitu. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema, kutokana na kile kilichotokea kwenye mazoezi ya Simba juzi, kikiwahusu wachezaji watatu wa timu hiyo, Emmanuel Okwi, Jjuuko Murushid na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Katika mazoezi hayo yanayoendelea katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, wachezaji hao walionyesha tukio lililowaacha midomo wazi baadhi ya waliolishuhudia.

Unataka kujua ilikuwaje? Ni hivi; wakati wachezaji waliohudhuria mazoezi ya siku hiyo asubuhi wakibadili nguo tayari kuanza programu za walimu wao, watatu hao walionekana kutegeana kufanya hivyo.

Wakati nyota wa timu hiyo kama John Bocco, Said Ndemla, Muzamiru Yassin, Mohammed Ibrahimu ‘ Mo’, Aishi Manula, Ally Shomary, Haruna Niyonzima, Shiza Kichuya, Nicolas Gyan, Laudit Mavugo na wengineo, wakibadili nguo tayari kuingia uwanjani, Okwi, Jjuuko na Tshabalala walijifanya wapo ‘busy’ wakiendelea na hamsini zao.

Wachezaji hao walikuwa ‘wakizuga’ kama hawafahamu kinachoendelea, wakiwaacha wenzao wakibadili nguo zao huku wao wakimbwilambwila kutokana na kile kilichoonekana kuviziana, kila mmoja akitaka kuwa wa mwisho.

Tukio hilo lilikuwa likifuatiliwa kwa karibu na BINGWA, ambapo mwisho wa siku, Okwi alibadili na kuingia uwanjani kabla ya kufuatiwa na Tshabalala, huku Jjuuko akiwa wa mwisho, ikiwa ni takribani dakika 15 tangu wenzake walipoingia dimbani.

Katika mazoezi hayo, Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog na msaidizi wake, Jackson Mayanja, walionekana kuwafungia kazi wachezaji wao kuanzia mabeki, viungo na washambuliaji, kuhakikisha hawafanyi makosa, lakini pia wanatumia kila nafasi watakayoipata.

Simba itavaana na Mwadui FC katika mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaokuwa ni wa tatu kwa Wekundu wa Msimbazi hao, ikiwa ni baada ya kuzivaa Ruvu Shooting waliyoichapa mabao 7-0, kabla ya kupata suluhu dhidi ya Azam Jumamosi iliyopita.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.