NEYMAR: SINA MPANGO NA BALLON D'OR

Bingwa - - MBELE -

PARIS, Ufaransa

STRAIKA wa Paris SaintGermain, Neymar, amezidi kusisitiza kwamba kutwaa ubingwa wa michuano mbalimbali ndilo jambo la muhimu kwake na wala hawazii kutwaa tuzo ya kwanza ya mchezaji bora wa dunia, Ballon d'Or.

Nyota huyo wa timu ya Taifa ya Brazil, alijiunga na matajiri hao wa Ufaransa akitokea Barcelona kwa ada ya Euro milioni 222 kiasi ambacho kilivunja rekodi ya usajili ya dunia na huku wengi wakibashiri kwamba amekikimbia kivuli cha Lionel Messi na changamoto ya kushindwa kutwaa tuzo hiyo binafsi.

Kujiunga na PSG kunatajwa na wengi kuwa kumemwongezea nafasi staa huyo kutwaa tuzo hiyo hususani baada ya kufunga mabao matano na huku akitoa pasi zilizozaa mengine mengi yakiwamo ya juzi ambayo PSG iliibuka na ushindi wa 5-0 dhidi ya Celtic katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hata hivyo, pamoja na kupewa nafasi hiyo, staa huyo wa zamani wa timu ya Santos, anasema ameelekeza nguvu zake ili kuhakikisha PSG inapata mafanikio na wala si kutwaa tuzo hiyo binafsi.

"Ni sawa mimi ni mwanasoka ambaye napenda kutwaa Ballon d'Or," alisema juzi mara baada ya mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa iliyofanyika mjini Glasgow.

"Lakini kwa sasa siliwazii hilo ila ninachokiwaza nikuhusu timu yetu kufanya vizuri kama timu na kama klabu,” aliongeza staa huyo.

Alisema kwamba, timu hiyo ni kubwa na kama wataendelea kufanya kama walivyofanya juzi wana nafasi ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.