Simba, Yanga kuzuia wachezaji kuzungumza linahitaji busara?

Bingwa - - MAONI MTAZAMO KATUNI -

HIVI karibuni Klabu za soka za Simba na Yanga ziliibuka na utaratibu wa ajabu kweli kwa kutangaza kuwapiga marufuku wachezaji wao kuzungumza na waandishi wa habari.

Wachezaji wa timu hizo kongwe wametangaziwa adhabu, ikiwamo kutozwa faini, endapo watagundulika kuzungumzia mambo ya klabu bila kupata idhini kutoka kwa viongozi wao.

Mpango uliopo ni kuona manahodha au ‘watakaoruhusiwa’ wakiwa wachezaji pekee wanaotakiwa kuzungumza na waandishi kuelekea au baada ya mchezo.

Ninauona uamuzi huo kuwa ni mwendelezo wa mazingira magumu ya utendaji kazi wa waandishi, hasa wa habari za michezo.

Hiyo ni mbali na usumbufu ambao wamekuwa wakiupata viwanjani na kutoka kwa viongozi na makocha ambao mara nyingi huwa hawatoi ushirikiano wa kutosha pale wanapoombwa kufanya hivyo.

Ni wazi utaratibu huo mpya ni wa kukurupuka na unapingana moja kwa moja na misingi ya weledi (professionalism), hasa ukizingatia umuhimu walionao waandishi katika safari ya maendelo ya mchezo huo wa soka hapa nchini.

Kwa kufanya hivyo, viongozi wa klabu hizo wamewakatili waandishi kwa kuwawekea mazingira magumu ya kumfikia mchezaji yeyote watakayemhitaji katika kazi zao. Huenda hilo limetokana na uelewa mdogo wa viongozi hao juu ya mchango wa waandishi katika mchezo wa soka hapa nchini na duniani kote.

Kwa kutojua au makusudi, wameuingilia uhuru wa waandishi katika ufanyaji kazi wao kwa kuwachagulia watu wa kuwapa habari.

Ikumbukwe kuwa, wachezaji ni chanzo kikubwa cha habari kwa waandishi, hasa katika mambo ya kiufundi. Baada ya benchi la ufundi, wachezaji wana uelewa mkubwa wa mambo ya kiufundi, hivyo waandishi wamekuwa wakiwategemea kupata mrejesho baada ya mechi au mazoezi.

Hivyo, sidhani kama ni busara kwa viongozi kuweka mpaka kati ya pande mbili hizo.

Lakini pia, waandishi wamekuwa wakiwategemea wachezaji kupata matatizo ya ndani ya klabu ambayo huenda ikawa si rahisi kwa viongozi kuyaweka hadharani.

Mfano; mara nyingi wachezaji wamekuwa wakiibua matatizo kama vile ukata, kutolipwa mishahara yao, kutelekezwa wanapokuwa majeruhi, tofauti zao na makocha, mambo ambayo ni ngumu kuona yakiwekwa hadharani na viongozi.

Viongozi wa Simba na Yanga wameupata wapi utaratibu huu ambao haupo kwenye ulimwengu wa soka? Katika nchi zilizopiga hatua kwenye mchezo huo, hasa zile za barani Ulaya, ambazo tumekuwa tukizitumia kama kiigizo, hilo halipo, kwani ni zaidi ya unyanyasaji kwa waandishi wa habari na hata kwa wachezaji.

Huko, huwezi kukuta wachezaji wakitozwa faini eti kwasababu wamezungumzia mchezo walioshinda, kupoteza au mambo mengine yanayoihusu klabu yao.

Ni kweli wapo ambao wamekuwa wakiadhibiwa kwa kuzungumza na waandishi, lakini si kwa kosa la kugusia mambo yanayoihusu timu, ikiwamo masuala ya kiufundi ambayo kwa hakika yanawahusu moja kwa moja.

Kwa nyakati tofauti, klabu za AC Milan, Newcastle, Manchester United ziliwahi kuwatoza faini mastaa Mario Baloteli, Joe Barton na Rio Ferdinand, baada ya kuwakashifu viongozi wao kupitia vyombo vya habari.

Hao walistahili adhabu kwa kutumia vibaya uhuru wao, lakini wasingekuwa hatiani eti kwa kuzungumzia mbinu za kiufundi za mchezo fulani.

Wenzetu wamekwenda mbali zaidi kwa hata kumruhusu mchezaji yeyote kutoa maoni yake juu ya mbinu za kocha na utendaji kazi wa benchi la ufundi.

Hivi karibuni, wakati wa sekeseke lake la kutaka kujiunga na Barcelona, staa Philipe Coutinho alitamka wazi kutofurahishwa na mbinu za kocha wake raia wa Ujerumani, Jurgen Klopp.

Nini kilifuata baada ya kauli hiyo? Coutinho alitozwa faini? Leo hii ni mmoja kati ya mastaa wa First eleven. Kwa Klopp na viongozi wa Liver, yale yalikuwa ni maoni ya Coutinho.

Lazima viongozi wa Simba na Yanga watumie busara katika uamuzi wao huo wa ajabu. Wakiwa ndiyo wadau wakubwa wa soka na michezo mingine, waandishi wanahitaji ushirikiano si tu kutoka kwa manahodha, bali kwa kila mchezaji wanayehisi ni chanzo kizuri cha habari fulani.

Kwa kutojua au makusudi, wameuingilia uhuru wa waandishi katika ufanyaji kazi wao kwa kuwachagulia watu wa kuwapa habari.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.