TIMU ZIIGE KWA NJOMBE MJI

Bingwa - - MAONI MTAZAMO KATUNI -

LIGI Kuu Tanzania Bara inatarajia kuendelea leo kwa mchezo kati ya wenyeji Azam dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Kesho ligi hiyo itaendelea katika viwanja vingine kwa Majimaji kuikaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, Mtibwa Sugar wakicheza na Mbao, Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro.

Mchezo mwingine utakuwa kati ya wenyeji Tanzania Prisons dhidi ya Ndanda kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na Lipuli watacheza na Ruvu Shooting, Uwanja wa Samora, wakati Singida United watakuwa nyumbani katika uwanja wao wa Jamhuri Dodoma kucheza na Stand United. Tukitarajia kuona kandanda safi, timu zinatakiwa kuiga mfano wa mashabiki wa Njombe Mji ambao walionyesha uzalendo wa hali ya juu wa kuishangilia timu yao ilipocheza na Yanga Jumapili iliyopita kwwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe.

Mashabiki wa Njombe Mji walionyesha kitu tofauti na ni nadra kukiona katika mikoa mingine, kwani waliacha kabisa ushabiki wa Simba na Yanga kwa kupigania ushindi wa timu yao.

Mara nyingi timu za Simba na Yanga zinapokwenda kucheza mikoani, zinapata sapoti kutoka kwa mashabiki wanaozipenda timu hizo, lakini kilichotokea Njombe ni tofauti kwao.

BINGWA tunawapongeza wakazi wa Njombe kutokana na uzalendo walioonyesha kwa timu yao, licha ya kufungwa bao 1-0 na Yanga.

Tofauti tuliyoona kwa wenyeji Njombe Mji ni ile ya kuweka pembeni u-Simba na u-Yanga na kuungana kitu kimoja kuishangilia timu yao huku wengi wakiwa wamevaa jezi ya timu yao kuonyesha uzalendo.

Huu tunaona ni uzalendo wa hali ya juu walioufanya wakazi wa Njombe, kwani baadhi ya mikoa imekuwa haitoi sapoti kubwa kwa timu za mikoa yao zinapocheza na Yanga na Simba, kwa kuwa wanakuwa ni sehemu ya mashabiki wa timu hizo.

Tunaamini kwamba, wakazi wengine wa mikoa mbalimbali wataiga uzalendo wa Njombe Mji na kwa kufanya hivyo ushindani wa soka Ligi Kuu Bara utaongezeka na bingwa atapatikana kutokana na uwezo wake.

Tunamaliza kwa kusisitiza kwamba, uzalendo walioonyesha wakazi wa Njombe uwe wa kuigwa kwa mashabiki wa mikoa mingine ili ushindani wa soka uwepo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.