TFFYAGAWAMIPIRA 100 MKOANI ARUSHA

Bingwa - - STORI ZA KITAA - NA JACKLINE LAIZER, ARUSHA

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetoa mipira 100 kwa Chama cha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA), kwa lengo la kuendeleza soka la vijana na wanawake hapa nchini.

Akizungumza wakati akikabidhi mipira hiyo kwa Katibu Mkuu wa ARFA, Zakayo Mjema wiki iliyopita, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa TFF, Sarah Chao, alisema lengo la kugawa mipira ni kutaka kuzalisha vipaji vingi vya soka.

"TFF ina dhamira ya dhati ya kuona mpira unachezwa kuanzia ngazi ya chini, hivyo ninaomba mipira hii ikatumike kama ilivyolengwa ili tuweze kuzalisha vipaji vya baadaye, kwani tukiwekeza katika soka la vijana wenye umri mdogo tutaweza kufanikiwa zaidi,” alisema Sarah.

Kwa upande wake, Mjema alisema wao kama viongozi wa ARFA watahakikisha mipira hiyo wanaigawa kwa uwiano sawa katika vyama vya soka vya wilaya.

Mjema alisema vyama hivyo vitagawa mipira hiyo kwa vituo vya kulelea vipaji chipukizi vya soka ‘Academy’ ili waweze kutimiza malengo ya shirikisho hilo.

"Kwa kweli ninaanza kuona mwanga wa mafanikio ya soka hapa mkoani kwetu, kama mnavyojua Mkoa wa Arusha ulivyodorora katika mchezo wa soka, tofauti na miaka ya nyuma ambapo mkoa huu ulikuwa wa kwanza kuwa na timu tatu zilizokuwa zinacheza Ligi Kuu.

Tulikuwa na timu ya AFC, JKT Oljoro na 977KJ, katika historia mkoa huu ndio chimbuko la soka la vijana hapa nchini," alisema Mjema.

Katika hatua nyingine, Mjema alisema wanatarajia kufanya mkutano mkuu kwa kuwashirikisha viongozi mbalimbali wa soka la vijana mkoani hapa, ili kupanga mikakati ya kuweza kufanikiwa katika kuendeleza soka la vijana.

Mjema alisema mkutano huo utapanga utaratibu wa kugawa mipira hiyo, iliyotolewa na shirikisho hilo. Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo Mkoa wa Arusha, ambaye ni Katibu Tawala (RAS), Richard Kwitega, alisema atahakikisha wanashirikiana bega kwa bega na uongozi wa ARFA kuhakikisha michezo, ikiwamo soka, inarudi katika kiwango chake kama miaka iliyopita.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.