Marcelo, Madrid kimeeleweka bwana

Bingwa - - SPORTS - MADRID, Hispania

HAKUNA mpango wa beki wa pembeni wa Real Madrid, Marcelo, kuikacha timu hiyo kama ilivyokuwa inaripotiwa hapo awali na hiyo ni baada ya Mbrazil huyo kusaini mkataba mpya wa miaka mitano na klabu hiyo.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, nyota huyo ameongeza mkataba wa kubaki Santiago Bernabeu hadi Juni 30, 2022.

Akiwa na Madrid tangu aliposajiliwa akitokea Fluminense mwaka 2007, Marcelo, mwenye umri wa miaka 29, ameshinda mataji 17, yakiwamo manne ya Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ na matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Taarifa ya kusaini mkataba mpya imekuja ikiwa ni baada ya Chama cha Soka nchini humo kumfungia mechi mbili kutokana na adhabu yake ya kadi nyekundu katika mchezo wa La Liga dhidi ya Levante, uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Nyota huyo alikumbana na adhabu hiyo baada ya kumpiga teke Jefferson Lerma, hivyo ataishia jukwaani wakati Madrid watakapozivaa Real Sociedad na Real Betis.

Marcelo ni mume wa mrembo Clarice Alves na ni baba wa watoto wawili, Enzo Gattuso Alves Vieira na Liam. Marafiki wake wakubwa ni Cristiano Ronaldo na Pepe.

Madrid hawajaanza vizuri safari yao ya kulitetea taji la La Liga msimu huu, kwani licha ya kuifunga Deportivo La Coruna katika mchezo wa ufunguzi, wamejikuta wakitoa sare katika michezo miwili iliyofuata dhidi ya Levante na Valencia.

Katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, wameanza vizuri kulisaka taji lao la 13 kwa kuisambaratisha Apoel mabao 3-0. Wakiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Bernabeu, Madrid walijipatia ushindi huo mnono kwa mabao ya Cristiano Ronaldo aliyefunga mawili na Sergio Ramos.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.