EPL mabingwa wa matumizi, La Liga wazee wa ‘kumeki’

Bingwa - - SPORTS -

DIRISHA la usajili katika ligi mbalimbali Ulaya lilihitimishwa rasmi wiki kadhaa zilizopita, huku ikishuhudiwa kila klabu ikifanikiwa kusajili wachezaji ambao ilikuwa ikiwafukuzia kwa muda mrefu.

Mbali na hilo, pia kuna nyingine ambazo zilishindwa kutimiza hazima yao, baada ya kuwakosa mastaa ambao zilikuwa zikitarajia kama wangeimarisha vikosi vyao.

Hata hivyo, baada ya kukamilika mchakato huo, swali ambalo lilikuwa limebaki ni kuhusu ligi gani ambayo imetumia kiasi kikubwa katika usajili huo.

Sasa swali hilo limepata ufumbuzi, baada ya Ligi Kuu England kubainika kuwa klabu zake ndizo zimetumia kiasi kikubwa cha fedha kuliko ligi yoyote kubwa barani Ulaya, huku Ligi Kuu ya Hispania, La Liga, ikifuatia kwa kuingiza kiasi kikubwa kutokana na mauzo ya wachezaji.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa jana na gazeti la Marca, tangu Juni mwaka huu wakati dirisha hilo lilipofunguliwa hadi Agosti lilipofungwa, jumla ya sajili 7,590 zilikamilika na takribani dola bilioni 4.71 zilitumika, kiasi ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na cha msimu uliopita.

Gazeti hilo likinukuu taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), vilevile zinaonesha kuwa, katika usajili huo ligi kubwa tano ambazo ni za Hispania, England, Ujerumani, Ufaransa na Italia, ndizo zilizochukua asilimia 21.2 ya usajili na huku pia zikinyakua asilimia 77.9 ya kiasi cha fedha zote zilizotumika.

Takwimu hizo zinaonesha pia kuwa, matumizi yote ya ligi hizo kubwa tano yameongezeka kutoka dola bilioni 1.2 zilizotumika mwaka 2012 hadi dola bilioni 3.67.

Katika kiasi hicho, Ligi Kuu England ndio walioteka soko baada ya kufanya uwekezaji wa dola bilioni 1.4 kwa ajili ya kununua wachezaji wapya, kiasi ambacho ni mara mbili ya kilichowahi kutumika katika Ligi Kuu ya Ufaransa, Ligue 1 katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Kwa upande wa Hispania, klabu za ligi hiyo zilitumia takribani dola milioni 763 na huku zikiingiza zaidi ya dola milioni 897.9 kutokana na mauzo ya wachezaji ambao ziliwauza katika ligi mbalimbali.

Kutokana na matumizi hayo, Shirikisho la Soka Ulaya, UEFA, kupitia kanuni yake ya kudhibiti matumizi makubwa katika soko la usajili, inaweza ikaichunguza ligi hiyo baada ya kutumia kiasi hicho kikubwa kwa mara nyingine na huku ikiingiza kidogo kutokana na mauzo iliyoyafanya.

Lukaku

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.