Wanaoiua tasnia ya burudani mitandaoni wanaachwaje salama?

Bingwa - - IJUMAA SPESHO - hassandaudi84@gmail.com HASSAN DAUDI 0746 252856

KWA miaka mingi sasa, nimekuwa mfuatiliaji mzuri wa tasnia ya burudani hapa nchini, hasa sanaa za muziki, uigizaji na mitindo, ambazo kwa sasa zimeonekana kupiga hatua kwa kiasi kikubwa.

Mbali na majukumu mengine niliyonayo, bado nimetenga sehemu ya muda wangu kufuatilia kila kinachotokea katika tasnia hiyo ambayo imekuwa chanzo cha ajira kwa kundi kubwa la vijana.

Huenda kama si hapa ilipofika tasnia ya burudani, leo hii lile linalotajwa kuwa ni janga la ukosefu wa ajira lingekuwa tishio zaidi. Umewahi kujiuliza hali ingekuwaje endapo mastaa wote tunaowaona na kuwasikia kupitia vituo vya televisheni na redio wangekuwa vijiweni leo hii wakiwa hawana kazi ya kufanya? Bila shaka ingekuwa balaa zaidi.

Katika miaka ya hivi karibuni, maendeleo ya sayansi na teknolojia yamekuwa na mchango mkubwa kwenye medani ya burudani. Ukweli ni kwamba, yamerahisisha kwa kiasi kikubwa upashanaji habari na matukio kati ya wasanii na mashabiki wao.

Kupitia mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Instagram, Whatsup na Youtube, imekuwa rahisi kwa wasanii kuwafikia mashabiki wao.

Siku mbili baada ya mwanamuziki Ali Kiba kuachia ngoma yake iitwayo Seduce Me, takribani mashabiki milioni mbili waliitazama video yake kupitia mtandao wa Youtube. Hicho ni kielelezo cha namna mitandao ya kijamii ilivyofanya kazi kubwa ya kuwaweka karibu wasanii na mashabiki wao.

Kwa mantiki hiyo, ni ngumu kuupa kisogo umuhimu wa mitandao ya kijamii katika kuiboresha tasnia ya burudani.

Hakuna ubishi kuwa mitandao ya kijamii na tasnia ya burudani ni pande mbili zinazoiunda sarafu moja.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni, mitandao ya kijamii imeonekana kutekwa na kundi la ‘wahuni’ wachache wanaojiita wanamitindo na ‘video vixen’. Kwa kutojua au makusudi, baadhi yao wamekuwa tatizo kwa tasnia ya burudani.

Wababaishaji hao wamekuwa wakitumia mwamvuli wa kazi hizo kufanya vitendo ambavyo kwa hakika vinaashiria kuishushia heshima tasnia ya burudani. Nikiwa sina sababu ya kuliweka hadharani jina lake, mmoja kati ya ‘virus’ hao aliwahi kushukiwa na mkongwe wa filamu za vichekesho nchini, Mzee Majuto.

Mzee Majuto alikemea vitendo vya mwanadada huyo kuvunja heshima ya tasnia ya burudani kwa tabia yake ya kuvaa vinguo vinavyouanika mwili wake.

Kama mwanadada huyo asingekuwa mwanamitindo na mwanamuziki, huenda nguli huyo angeachana naye na wala asingemzungumzia. Tatizo alilokuwa ameliona Mzee Majuto ni kwamba, uchafu wa msichana huyo uliihusu tasnia ya burudani kwa ujumla.

Ni kweli ili kuwa video vixen wa kiwango cha kimataifa, unapaswa kuwa na tabia za kupiga picha za utupu na kuzitupia mitandaoni? Siamini.

Kwanini wahusika (wasanii na wadau) wa tasnia ya burudani wamelichukulia poa suala hili la kuzuka kwa wahuni wanaoianika miili yao mitandaoni wakijiita wanamitindo, wanamuziki au waigizaji?

Kupitia uchafu wao uliotapakaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwamo kunengua nusu utupu, si rahisi kuwashawishi wazazi wawaruhusu mabinti zao kujiingiza katika ulimwengu wa burudani.

Huenda tukarudi kule tulikokuwa miaka ya 1990 ambapo tasnia ya burudani ilionekana kuwa chanzo kikubwa cha kupotea kimaadili kwa vijana wa Tanzania. Haikuwa rahisi kwa mzazi kukubali mtoto wake ajiingize kwenye muziki au uigizaji kwani sanaa hizo zilionekana kujaa upotoshaji.

Lakini je, mamlaka ambazo zimekuwa zikizuia video na audio zisizo na maadaili kupata nafasi kwenye vituo vya televisheni na redio zimeliona hilo? Kuna mpango wowote uliopo kuhakikisha zinakomesha uhuni huo unaoendelea kushika kasi kwenye mitandao ya kijamii?

Ifahamike kuwa wanaojiita wanamuziki, waigizaji au wanamitindo na kufanya vitendo viovu ni sehemu ya tasnia ya burudani, hivyo madudu yao yanachangia kwa kiasi kikubwa kuwaharibia wenzao wanaozifanya kazi hizo.

Mbali na kuwachafua wasanii wengine, pia wanavunja maadili, jambo ambalo linauweka hatarini utamaduni wa Tanzania, hasa mbele ya macho ya jamii nyingine zinalitaja kuwa ni Taifa lililostaarabika.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.