ZINGATIA FURAHA YAKO KABLA HUJAINGIA KATIKA UHUSIANO

Bingwa - - MAKALA -

SI kwa sababu ya umri ila ni kwa ajili ya uamuzi wao na mienendo yao, vijana linabaki kuwa kundi lenye kuathirika zaidi na maumivu na shida za mapenzi kuliko rika lingine.

Japo mapenzi ni suala linalogusa nyanja zote. Kuanzia vijana mpaka watu wazima na wazee, ila vijana wanaishi katika mateso makubwa ya mapenzi kuliko makundi mengine.

Kushindwa kujitambua na kutambua thamani yao imo, ila pia kupenda kuchukua maamuzi ya haraka bila kufikiri mara mbili huenda ndiyo ikawa sababu kuu. Tujiulize haya.

Ni mara ngapi umeweza kuwaona vijana wakipeana namba za simu kwa ajili ya kutafutiana wapenzi? Ni mara ngapi umeshuhudia wavulana wakionesha kubabaishwa sana na umbile na sura za wasichana kiasi cha kutaka kuoa kwa sifa hizo za nje pekee?

Si ajabu katika maongezi yao, mmoja akatoa namba na kusema: “Hii ni ya demu fulani mkali sana, mtafute uone.” Baada ya hapo mhusika anamtafuta msichana huyo na kwa muda mfupi baadaye wanakuwa katika uhusiano kwa vigezo vya sura zao na vipato vyao. Kisha baadaye wanaingia katika ndoa. Ndoa yao ikitawaliwa na mateso pamoja na mambo mengine ya kutisha, wanaanza kulia na kusema mapenzi mabaya.

Wengine hata katika matembezi ya kawaida tu anaweza kukutana na mvulana mtanashati au msichana mrembo, akataka kuingia naye katika uhusiano.

Kwa mavazi na mwonekano wake, bila kujali vingine zaidi, anamwona anafaa na si ajabu siku chache mbele akahitaji kuishi naye. Katika aina hii ya maisha kweli furaha unayoihitaji katika uhusiano inaweza kupatikana? Thubutuu!

Kwa uzuri wake, kwa gari yake afae kuwa na wewe katika maisha? Ni kweli itakuwa rahisi kuepukana na maumivu katika uhusiano wako?

Mapenzi si suala la bahati sana. Mapenzi ni suala la umakini na uvumilivu. Isitoshe sura yake kukufanya kuwa naye katika maisha, utajuta.

Hata kama anapendeza vipi, ila unapaswa kuwa makini kabla hujaingia naye katika uhusiano. Mapenzi si suala la mchezo hata kidogo. Funua macho na akili yako kuona ambayo wengi hawayaoni.

Sisemi usiwe na mwanamke anayekuvutia ama mwanaume mwenye vigezo unavyotaka. Usinielewe vibaya. Pointi yangu hapa ni hatua gani unapitia katika kuwa na mtu unayemhitaji?

Mapenzi si suala la nguo wala magari. Ni suala la kihisia na furaha ya maisha yako. Ndiyo, kwa macho unaweza kuona kuwa anafaa, ila je, una hakika kweli ukiwa naye atakufanya uone na kujivunia thamani yako? Ndani ya magari ya thamani wengi wanalia na mapenzi.

Katika majumba makubwa na ya gharama ila wengi bado wanateseka kwa sababu ya mapenzi. Acha kukurupuka. Muangalie huyo unayetaka kuwa naye, kisha tafakari maisha yako ya baadaye.Je, unamhitaji mtu wa aina hiyo? Je, umemwangalia vizuri tabia, mienendo na kujua hisia zake vema hata uone kwamba ukiwa naye utakuwa mtu mwenye amani na raha katika maisha?

Katika maisha unadhani kipi bora? Kati ya furaha ya nafsi au sifa ya kuwa na fulani mwenye gari, nyumba na mashamba mengi ila anakunyima furaha ya maisha?

Usicheze kamari katika uhusiano wako. Mapenzi yako ni maisha yako. Unaweza kuwa na amani na furaha kama ukiamua. Na unaweza kuishi kwa mashaka ikiwa pia utaamua.

Suala ni kutuliza akili na kupima mambo yako. Jipe muda wa kumtafakari huyo anayekwambia anakupenda. Huenda ikawa kweli anakupenda ila pia huenda ikawa si kweli. Jipe muda wa kumsoma na kumjua vizuri.

Acha kufanya uamuzi kana kwamba unamkomoa mtu. Mapenzi ni maisha yako. Yanaweza kukupa furaha na kukupa huzuni pia. Hivyo katika suala la kumkataa mtu au kumkubali inabidi uangalie hayo kwanza.

Si kutaka kumkomoa mtu wala kumfurahisha mtu. Mapenzi ni yako. Ni maisha yako na furaha au huzuni yako.

Epuka sana kuwa na mtu kwa sababu anasifiwa na watu. Kuwa na mtu kwa sababu ya vigezo vyako huku hali ya furaha na amani yako ikiwa ndiyo kipaumbele cha kwanza katika uamuzi wako.

Bila umakini na busara unaweza kudhani unamkomoa fulani kumbe unatengeneza janga mwenyewe katika maisha yako.

Unadhani nini bora katika uhusiano wako? Ni furaha na amani au gari na sifa za kuwa uko na fulani mzuri wa sura au maridadi wa umbile?

Maisha yako yanahitaji furaha na amani, gari na nyumba nzuri vinaweza visichochee fahari ya kuvimiliki kama huna amani na furaha katika maisha yako.

Kama unaingia katika uhusiano na mtu asiyekujali na kukuthamini hayo magari na nyumba yatakufaa nini? Ana magari mengi ila kila siku yanabeba mahawara!

Ana sura nzuri na umbile la kibantu ila kila siku anakusaliti! Raha ya kuwa naye iko wapi sasa? Furaha yako inaletwa na thamani yake kwako pamoja na heshima na si gari lake wala nyumba anayomiliki.

Nyumba na gari vinabaki kuwa vyake ila umuhimu wako inabidi uonekane kwa kukufanya kuwa na amani na furaha katika maisha yako. Mapenzi bila furaha hayana maana tena. Bila kujaliana na kuthaminiana hakuna haja ya kuyasifu mahusiano yako.Kuwa makini katika maamuzi yako. Kwani kwayo kuna raha na maumivu yako. Kauli yako juu ya huyo anayekutaka inaweza kuwa ni kauli ya ushindi wa furaha katika nafsi yako au ikawa kauli ya maumivu na hangaiko la moyo wako. Kabla hujakubali wala kukataa kuwa makini. Tena uwe makini sana.

Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya ushauri wa uhusiano, maisha na utulivu wa hisia

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.