Msuva kuoga minoti Uarabuni

Bingwa - - HABARI /TANGAZO - NA SALMA MPELI

WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva, anatarajia kupata fedha zake za usajili kutoka kwenye klabu yake mpya ya Difaa el Jadida inayoshiriki Ligi Kuu ya Morocco.

Mchezaji huyo wa zamani wa Yanga, alijiunga na klabu hiyo Julai mwaka huu kwa mkataba wa miaka mitatu kwa dau la Sh milioni 300 ambalo limegawanywa kwa timu yake ya zamani na mchezaji binafsi.

Mbali na dau hilo la usajili, pia mchezaji huyo alipewa ofa ya mshahara wa Sh milioni tisa kwa mwezi, mara mbili ya ule aliokuwa anaupata alipokuwa kwenye klabu ya Yanga.

Akizungumza na BINGWA hivi karibuni, baba mzazi wa winga huyo machachari, Happy God Msuva, alisema kuwa hadi sasa mwanawe hajalipwa fedha zake hizo za usajili lakini hiyo ni kutokana na kutokuwa na kibali cha muda mrefu cha kufanya kazi nchini Morocco.

Alisema kwa sasa mchezaji huyo anatumia kibali cha muda mfupi ambacho kisheria hawezi kuingiza fedha zake hizo, hivyo klabu yake hiyo mpya ipo katika mchakato wa kuhakikisha kibali cha kufanya kazi kwa miaka mitatu nchini humo kinapatikana ili waweze kumlipa fedha zake.

“Tupo mwanangu bado anasubiri fedha zake za usajili kule Morocco, kwani walishindwa kumlipa kwa wakati kutokana na kutokuwa na kibali cha kufanya kazi nchini humo kwa miaka mitatu, lakini ndiyo wapo katika mchakato wa kushughulikia jambo hilo ambapo si muda mrefu litakamilika,” alisema baba yake Msuva.

Kutokana na jambo hilo, mchakato huo utakapokamilika muda si mrefu akaunti ya mchezaji huyo itatuna baada ya kuingiziwa fedha zake.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.