NDUGU WA AVEVA, KABURU WAANGUA KILIO MAHAKAMANI

Bingwa - - HABARI /TANGAZO - NA KULWA MZEE

NDUGU na jamaa wa Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange maarufu kama Kaburu, wamejikuta wakitiririkwa na machozi baada ya Jamhuri kueleza kwamba upelelezi wa kesi yao ya kutakatisha fedha haujakamilika.

Jamhuri ikiwakilishwa na Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, alidai jalada la kesi hiyo bado liko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Swai alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.

Alidai baada ya Takukuru kukamilisha uchunguzi walipeleka jalada hilo kwa DPP ili kuangalia kama upelelezi unakidhi kulingana na kesi iliyopo mahakamani ama la.

Wakili huyo aliomba kuahirisha kesi hiyo na mahakama ilikubali kuahirisha hadi Oktoba 25, mwaka huu.

Baada ya Hakimu Nongwa kuahirisha na washtakiwa kurudi mahabusu, ndugu na jamaa waliokuwepo katika ukumbi wa mahakama ya wazi namba moja walitoka huku wakiwa na huzuni.

Baadhi walipumzika katika benchi nje ya ukumbi huo wa mahakama huku mmoja wao akiwa anafuta machozi na wengine waliosimama walikuwa wakimfariji kwa kumpigapiga mabega mwenzao.

Wakati akiendelea kufarijiwa miongoni mwa wanaomfariji alishindwa kuvumilia akaamua kusogea pembeni, aliinua shati yake na kuanza kujifuta machozi.

Aveva na Nyange wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha Dola 300,000 za Marekani.

Washtakiwa wapo rumande kwa sababu shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.