KMC ya Minziro yalizwa Dar

Bingwa - - HABARI /TANGAZO - NA TIMA SIKILO

TIMU ya Ngorongoro Heroes imeibuka kidedea kwa kuinyuka KMC mabao 2-1 katika mchezo wa kirafiki uliochezwa jana asubuhi katika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Mchezo huo ulianza kwa kasi kila timu ikiwa na shauku ya kuanza kuliona lango la mpinzani wake, ambapo ilikuwa ni KMC iliyocheka na nyavu za Ngorongoro Heroes dakika ya 25 kupitia Khalfan Kigozi.

Dakika tano baadaye, Ngorongoro Heroes walifanya shambulizi kali lililowawezesha kusawazisha bao hilo kupitia Mohammed Abdallah.

Lakini wakati mashabiki waliofika uwanjani hapo kushuhudia mtanange huo wakidhani ungemalizika kwa sare ya bao 1-1, Ibrahim Abdallah aliifungia Ngorongoro bao la pili na la ushindi dakika moja kabla ya kuhitimishwa kwa mchezo huo.

Mchezo huo ulikuwa mkali kwa timu zote mbili kucheza soka la uhakika na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara.

Hata hivyo, Ngorongoro Heroes ndio walioonekana kuumiliki zaidi mchezo huo, japo KMC inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Fred Felix Minziro, nayo ilionyesha kiwango kizuri.

Baada ya mchezo huo, Ngorongoro Heroes walicheza mchezo mwingine wa kirafiki kwenye uwanja huo dhidi ya timu ya JKU inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar, ambapo mtanange huo ulimalizika kwa suluhu.

Minziro

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.