Hali ikiwa hivi bora Mkude aondoke Simba

Bingwa - - MAONI MTAZAMO KATUNI -

NAHODHA wa zamani wa Simba, Jonas Mkude, anapitia kipindi kigumu ambacho hajawahi kukutana nacho kutokana na kukaa benchi kwa muda mrefu, huku mengi yakizungumzwa kwamba huenda kuna mkono wa mtu ndani yake.

Mkude alianza kuvuliwa kitambaa cha unahodha wakati timu hiyo ikiwa kambini nchini Afrika Kusini na kukabidhiwa Method Mwanjale, huku wasaidizi wake wakiwa John Bocco na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Kuvuliwa unahodha kwa Mkude kulizua maswali mengi miongoni mwa wadau wa soka, wengine wakidai kwamba ni kutokana na utovu wa nidhamu huku baadhi wakidai ni mizengwe anayofanyiwa na baadhi ya viongozi na wengine wakisema ni maamuzi ya benchi la ufundi na lazima yaheshimiwe.

Wanaodai kwamba huenda ni kutokana na utovu wa nidhamu wanaenda sambamba na wale wanaosema anawekewa mizengwe, kwani wote kauli yao ni ile kwamba kama si hivyo isingekuwa rahisi avuliwe unahodha na kunyimwa hata usaidizi.

Taarifa nyingine zisizo rasmi ambazo zimezagaa mtaani zinadai kwamba anachofanyiwa Mkude kinatokana na yeye kuamua kusaini mkataba mpya aliyekwenda moja kwa moja kwa Mohamed Dewji ‘MO’, bila kupitia kwa wale ambao wanajifanya ndio wenye timu.

Taarifa hizo zinadai kwamba, awali Mkude alikataa kusaini mpaka pale MO alipomuita mezani wakamalizana wenyewe, kitu ambacho kinadaiwa kiliwakera baadhi ya viongozi na wakaamua kutoa maelekezo kwa benchi la ufundi.

Hizo ni taarifa ambazo zimezagaa mitaani zikizidi kuwachanganya mashabiki wa klabu hiyo ambao wana mapenzi mema na Mkude, wakikumbuka mchango mkubwa alioutoa tangu alipotoka kikosi B, mpaka kupata unahodha kikosi cha kwanza.

Kwa sasa Mkude yule ambaye alikuwa hakosi kwenye kikosi cha kwanza, amekuwa mtokea benchi na kama ataingia basi ni zile dakika za lala salama, kitu ambacho kinaweza kumpoteza kabisa na kama hatashtuka anaweza akajikuta anastaafu akiwa bado mbichi.

Kinachoweza kumuumiza zaidi Mkude, ni kwamba James Kotei ambaye ndiye chaguo la kwanza la kocha Joseph Omog, amekomaa kwelikweli kitu ambacho kinaweza kumfanya Mtanzania huyo kujikuta akitokea benchi kila mara.

Athari ya kwanza ambayo imeanza kumtokea Mkude ni kwamba haitwi tena kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, kutokana na kutotumika pale Simba na kwa jinsi hali inavyokwenda anaweza akasahaulika kabisa.

Hiyo inamaanisha kwamba hata kama Mkude anazo ndoto za kucheza soka la kulipwa, itamuwia vigumu kwenda kwani kama hatumiki kwenye timu yake ni wapi wanaweza

kumuona na kumsajili? Labda asajiliwe hapahapa nchini na timu kama Majimaji, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na nyingine.

Katika michezo mitano ambayo Simba wamecheza mpaka sasa, Mkude hajatumika ipasavyo, kwani amecheza michezo miwili tu tena dakika zile za mwisho hiyo ikimaanisha kwamba mwendo ukiwa hivyo atapotea kabisa vinginevyo binafsi namshauri akiona mambo magumu afadhali atafute namna nyingine ikiwamo kuondoka.

Mkude bado ni kijana mdogo ambaye anatakiwa atumike ipasavyo, sasa kama ataendelea kuwa chini ya Omog, anaweza akapoteza dira na mwisho wa siku malengo yake yakashindwa kutimia.

Ninachoweza kumshauri Mkude ni kwamba apambane kupata namba ikishindikana amfuate mwenzake Ibrahim Ajib kule Yanga kwani hawawezi kumnyima nafasi.

Hapa namaanisha kwamba kama kikwazo cha Mkude kutokupata namba ni kutokana na Kotei, basi apambane kisawasawa lakini kama ni hizo tuhuma nyingine za kwamba kuna baadhi ya viongozi wanamchukia kwa sababu zile fedha za usajili hazikupitia mikononi mwao wakaamua wamshughulikie kwa njia hii, ni bora atimke aisee.

Mkude bado ni kijana mdogo ambaye anatakiwa atumike ipasavyo, sasa kama ataendelea kuwa chini ya Omog

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.