BODI YA LIGI IENDELEE KUCHUKUA HATUA

Bingwa - - MAONI MTAZAMO KATUNI -

KAMATI ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, imemuondoa mwamuzi msaidizi, Grace Wamara kuchezesha Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kukosa umakini na kusababisha kukubali bao lenye utata la Stand United dhidi ya Mbeya City.

Katika mchezo huo uliochezwa Septemba 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, wenyeji Stand United waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Kutokana na sababu hiyo, mwamuzi Wamara amerejeshwa katika Kamati ya Waamuzi ya TFF kwa ajili ya hatua zaidi aliyeondolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(5) ya ligi kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.

Mwamuzi mwingine aliyeondolewa kwenye orodha ya kuchezesha michezo ya Ligi Daraja la Kwanza ni Youngman Malagila kutokana na kuchezesha chini ya kiwango mechi kati ya Rhino Rangers na JKT Oljoro iliyofanyika Septemba 30, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

Kamati ya Bodi ya Uendeshaji wa Ligi ilichukua hatua kwa mwamuzi wengine, Steven Patrick na msaidizi wake, Adrian Kalisa waliochezesha mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza kati ya Pamba na Biashara United uliochezwa Oktoba 2, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Nyamagana.

Makosa yaliyosababisha kuwaondoa waamuzi hao yanafafana kwani sababu kubwa iliyoelezwa ni kukosa umakini na kuchezesha chini ya kiwango.

Kwanza tunaipongeza Kamati ya Bodi ya Uendeshaji Ligi kwa kuwa umakini wa kufuatia matukio mbalimbali yanayojitokeza uwanjani na kutolewa uamuzi haraka.

Tunaamini kwamba uamuzi wa kuwaondoa na kuwapa adhabu baadhi ya waamuzi, wachezaji na makocha na viongozi unaweze kupunguza matukio yasiyofaa katika Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na Daraja la Pili.

Tunasema kwamba, Kamati ya Bodi na Uendeshaji Ligi iendelee kusimamia kanuni za ligi hiyo ili kuweza kumpata bingwa pasipo na malalamiko ya upendeleo.

Kamati ya Bodi ya Uendeshaji Ligi inafanya kazi kwa kuzingatia kanuni, hivyo isione aibu kumchukulia maamuzi, mchezaji, kocha na viongozi wa klabu ambaye atakwenda kinyume na kanuni walizojiwekea katika kusimamia mpira.

BINGWA tunasema kwamba ili mpira uweze kuchezwa ni lazima sheria 17 za soka, utaratibu na kanuni zifuatwe kwa kila mmoja.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.