SIMBA 'WAMFICHA' KAMUSOKO DAR

Bingwa - - MBELE - HUSSEIN OMAR NA EZEKIEL TENDWA

UKISEMA Simba wamemficha kiungo wa Yanga, Thaban Kamusoko, utakuwa hujakosea

UKISEMA Simba wamemficha kiungo wa Yanga, Thaban Kamusoko, utakuwa hujakosea kwani licha ya kwamba hajaambatana na timu kwenda kuwakabili Kagera Sugar mkoani Kagera kutokana na majeraha yanayomkabili, lakini ukweli ni kwamba anaandaliwa kwa ajili ya mchezo dhidi ya watani wao hao wa jadi.

Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana Oktoba 28, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ambapo tayari presha imeanza kupanda kwa pande zote licha ya kwamba timu hizo zina michezo miwili kila moja kabla ya kukutana.

Yanga watacheza na Kagera Sugar na Stand United ndipo wakutane na Simba na kwamba taarifa kutoka ndani ya kikosi hicho, zinadai kwamba hawataki kumchosha Kamusoko katika mechi hizo ili wakikutana na watani zao wa jadi, awe fiti asilimia 100.

Mbali na Kamusoko, pia mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, leo watashindwa kusafiri na straika wao Donald Ngoma, ambaye naye anakabiliwa na majeraha na taarifa zaidi zinadai kuwa mpaka siku ya mchezo dhidi ya Simba, atakuwa fiti hiyo ikimaanisha kwamba kocha George Lwandamina anaficha silaha zake.

Wajangwani hao wanakwea pipa leo kuwafuata Kagera Sugar na baadaye kwenda Shinyanga kucheza na Stand United, bila kuambatana na wachezaji hao wawili na baada ya michezo hiyo, ndipo sasa watakoki silaha zao kuwasubiri Simba.

Ngoma na Kamusoko wamepewa wiki moja zaidi ya mapumziko, huku wakiwa chini ya uangalizi wa daktari kufuatia straika huyo kusumbuliwa na nyama za paja huku Kamusoko akisumbuliwa na goti.

Nyota hao waliumia hivi karibuni ambapo benchi la ufundi la timu hiyo pamoja na daktari wamelazimika kuwapa siku saba kwa ajili ya mapumziko ili kuangalia afya zao kabla ya kuanza mazoezi mepesi ya kuwawinda Simba.

Kigogo mmoja wa Yanga ameliambia BINGWA, kwamba wanautolea macho yote mchezo huo dhidi ya Simba utakaochezwa Oktoba 28, ndiyo maana hawataki kuwachoshwa Kamusoko na Ngoma na badala yake wanawaandaa kwa ajili ya Wekundu hao wa msimbazi.

“Tumekuwa na tatizo la baadhi ya wachezaji wetu kuwa majeruhi na sasa tumeamua kuwa na tahadhari kubwa ikizingatiwa kwamba tunao mchezo mgumu mbele yetu dhidi ya Simba, ndiyo maana hawa akina Ngoma na Kamusoko hatutaki kuwachosha,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, itakuwa vigumu kwa Ngoma na Kamusoko kuwatumia kwenye michezo yao miwili dhidi ya Kagera Sugar na Stand United na badala yake wanaandaliwa kwa ajili ya kuwakabili Simba.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.