Majembe 11 usingependa yakosekane Kombe la Dunia 2018

Bingwa - - MBELE -

MASTAA Alexis Sanchez na Gareth Bale, ni kati ya majina ambayo yatakosekana katika fainali za Kombe la Dunia za majira ya joto yajayo, baada ya mataifa yao kushindwa kufuzu michuano hiyo.

Sanchez atazikosa fainali hizo baada ya Chile kuchapwa mabao 3-0 na Brazil wakati Bale hataonekana naye baada ya Wales kuchapwa bao 1-0 wakiwa nyumbani na Jamhuri ya Ireland.

Hata hivyo, pamoja na nyota hao kukosekana pia kuna orodha kubwa ya wachezaji wengi wenye majina ambao hawatakuwamo kwenye fainali hizo.

Katika makala haya, BINGWA limejaribu kuangalia kikosi cha wachezaji 11 ambacho pengine usingependa sura zao zikosekane.

Mlinda mlango, Jan Oblak (Slovenia/Atletico Madrid)

Akiwa ameshatangazwa kuwa mlinda mlango bora wa michuano ya La Liga, kipindi cha miaka miwili iliyopita, matumaini ya staa huyo mwenye umri wa miaka 24 ya kushiriki fainali hizo yalitoka juzi, baada ya Slovenia kushindwa kufuzu kupitia kundi ambalo mshindi aliibuka kuwa England.

Beki wa kulia: Antonio Valencia (Ecuador/Manchester United)

Kiwango kizuri alichokionesha katika safu ya ulinzi ya kulia msimu uliopita, Valencia alitangazwa kuwa mchezaji bora wa klabu hiyo ya Old Trafford hata hivyo staa huyo naye hataweza kushiriki baada ya Ecuador kushindwa kutinga hatua hiyo ambayo nchi hiyo ingekuwa ni mara yake ya tatu kushiriki.

BEKI WA KATI: VIRGIL (HOLLAND/ SOUTHAMPTON)

Licha ya Van Dijk kuwa ameshaweka wazi kuwa anataka kuitema klabu hiyo ya St Mary's, lakini bado ataendelea kuitumikia hadi Juni mwakani, lakini vile vile naye atakosa nafasi ya kuonesha kipaji chake katika michuano hiyo mikubwa baada ya Uholanzi kushika nafasi ya tatu ya Kundi A. BEKI WA KATI: GARY MEDEL (CHILE/ BESIKTAS)

Staa huyo wa zamani wa timu za Sevilla na Inter Milan, alikuwa akijitolea kwa hali na mali akiwa katika uzi wa timu hizo.

Hata hivyo, pamoja na kucheza kwa kiwango cha hali ya juu, lakini ameshindwa kuliwezesha taifa lake kufuzu fainali hizo baada ya kushika nafasi ya nne kutokana na kipigo ilichokipata kutoka kwa Peru.

Beki wa kulia: David Alaba (Austria/ Bayern Munich)

Kwa kufanikiwa kutwaa mara sita ubingwa wa michuano ya Bundesliga na wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, ilikuwa imeshadhihirisha wazi kuwa Alaba atakuwa na nafasi kwenye kikosi cha nchi yake.

Hata hivyo, staa huyo wa timu ya Taifa ya Austria, amebaki na uzoefu wa kucheza fainali za Euro 2016 tu.

KIUNGO WA KATI: NABY KEITA (GUINEA/RB LEIPZIG)

Kwa sasa Liverpool huenda wakawa wanafurahi kuwa kiungo huyo atatua Anfield majira ya joto yajayo akiwa fiti baada ya Guinea kushindwa kufuzu fainali hizo kupitia kundi lililokuwa na timu za Tunisia, Jamhuri ya Kidemorasi ya Kongo (DRC) na Libya.

KIUNGO WA KATI: ARTURO VIDAL (CHILE/BAYERN MUNICH)

Kiungo huyo ambaye aling’ara fainali mbili za Kombe la Dunia alikuwa amefungiwa mechi ya mwisho ya Chile dhidi ya Brazil na juzi alionekana kuchoka baada ya timu hiyo ya taifa kutupwa nje.

STRAIKA WA PEMBENI KULIA: GARETH BALE (WALES/REAL MADRID)

Kulikuwapo na mtazamo tofauti miaka michache ya nyuma kuhusu uwezo wa Wales. Lakini hata hivyo baada ya kufanikiwa kutinga nusu fainali ya Euro 2016, ikaonekana kama ingekuwa mara yake ya kwanza kwa Bale kucheza fainali hizo za dunia, lakini cha kushangaza wakajikuta wakiduwazwa na Jamhuri ya Ireland.

STRAIKA WA PEMBENI KUSHOTO: ARJEN ROBBEN (HOLLAND/BAYERN MUNICH)

Mkongwe huyo juzi alitangaza kustaafu kuchezea timu hiyo ya taifa baada ya Uholanzi kuchapwa na Chile wakiwa nyumbani.

STRAIKA: ALEXIS SANCHEZ (CHILE/ ARSENAL)

Chile walipoteza nafasi yao dakika za mwisho wakati Peru ilipofanikiwa kusawazisha dhidi ya Colombia, hivyo nyota huyo wa Arsenal hataweza kuonesha makali yake akiwa na La Roja.

STRAIKA: PIERRE-EMERICK AUBAMEYANG (GABON/BORUSSIA DORTMUND)

Gabon haijawahi kufuzu fainali za Kombe la Dunia na hivyo nyota wake, Aubameyang, huenda kamwe hasiweze kushiriki hata mara moja.

WACHEZAJI WA AKIBA: Jasper Cillessen (Holland/Barcelona) Daley Blind (Holland/Manchester United) Miralem Pjanic (Bosnia and Herzegovina/Juventus) Marek Hamsik (Slovakia/Napoli)

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.