HANS PLUIJM AIGWAYA YANGA

Bingwa - - MBELE - NA HUSSEIN OMAR

KOCHA wa Singida United, Hans van der Pluijm, amesema hana habari na kinachoendelea katika kikosi chake cha zamani cha Yanga na badala yake ameelekeza nguvu zake zote kuipa ubingwa timu yake hiyo mpya.

Kocha huyo aligoma kuzungumzia chochote juu ya mwenendo wa Yanga kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambao wanaonekana kusuasua msimu huu.

Pluijm aliyeipa Yanga mataji kibao na kuifikisha katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa misimu miwili aliyokaa kwenye benchi la ufundi la timu hiyo, alisema anachotaka ni kuona Singida United inapata mafanikio na si kuizungumzia Yanga au timu yoyote ile.

“Sitaki kuwa sehemu ya mazungumzo ya Yanga, nataka Singida ndio iwe inazungumziwa kutokana na mafanikio yake. Hilo ndilo jambo muhimu kwangu. Maendeleo ya wachezaji na kiwango kizuri cha timu,” alisema.

Alipoulizwa anazungumziaje uhaba wa mabao katika kikosi cha Yanga, Plujim alisema: “Sitaki kuligusia hilo. Tafadhali, hiyo si timu yangu. Wewe niulize kuhusu Singida.

“Sitaizungumzia Yanga kwa sababu si sehemu ya majukumu yangu. Unatakiwa kulielewa hilo.”

Pluijm alisisitiza kuwa amedhamiria kuandika historia mwaka huu na kuwaonyesha mashabiki na wapenzi wa soka hapa nchini kuwa yeye ni nani kwa kuipa mafanikio makubwa Singinda United.

“Sina presha huku nipo natengeneza timu ya ushindani itakayokuwa tishio ndani na nje ya nchi, natengeneza vipaji vya hali ya juu kwa maendeleo ya timu,” alisema Pluijm.

Kwenye msimamo wa Ligi Kuu, Singida United inakamata nafasi ya nne baada ya kujikusanyia pointi 10 huku ikishuka uwanjani mara tano.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.