Simba: Mtibwa haituumizi kichwa

MWAKYEMBE AMALIZA MCHEZO

Bingwa - - MBELE -

NA ZAITUNI KIBWANA

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, jana amekutana na viongozi wa klabu ya Simba na aliyekuwa mdhamini wa klabu hiyo, Hamisi Kilomoni, kuzungumza mambo mbalimbali, ikiwamo mgogoro uliopo kati yao.

Kilomoni aliingia kwenye mgogoro na viongozi wa Simba baada kwenda mahakamani kupinga Mkutano Mkuu wa mabadiliko ya katiba, ambao hata hivyo ulifanyika na kumwondoa kwenye bodi ya Baraza la Wadhamini.

Akithibitisha kufanyika kwa kikao hicho, Ofisa Michezo wa Wizara hiyo, Anita Jonas, alisema Waziri aliwaita pande zote mbili kwa mazungumzo binafsi ambayo hayapaswi kuwekwa hadharani.

“Ni kweli Waziri Mwakyembe alikutana na viongozi wa pande hizo mbili ambao ni Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ na Hamis Kilomoni, sambamba na watendaji wengine wa klabu, lakini mazungumzo yalikuwa ni yao binafsi,” alisema.

Hata hivyo, licha ya Anita kushindwa kuweka wazi kilichozungumzwa, ukurasa wa Wizara ya Habari uliandika jana kuwa: “Waziri Mwakyembe amewataka viongozi wa Simba kuungana kwa manufaa yao pamoja na kuzingatia uwekezaji wenye tija. Gazeti la BINGWA pia lilimtafuta Kaimu Rais huyo, ambaye alithibitisha kufanya mazungumzo na Waziri Mwakyembe na kudai kuwa lengo lilikuwa ni upatanisho kati yao.

“Ulivyosikia ndio ukweli, tulikutana na Waziri Mwakyembe na kilichofanyika ni upatanisho wa pande hizi mbili tu, mengine waulize Wizara ya Habari,” alisema Try Again.

Try Again alipoulizwa kuhusu kinachofuata baada ya kikao hicho, alitoa maelekezo kuwa atafutwe Katibu Mkuu, Dk. Arnold Kashembe, ili afafanue zaidi kilichojiri katika mazungumzo yao na waziri.

Simba iliingia katika mgogoro na mdhamini wao huyo baada ya kutaka kubadilisha katiba ya klabu hiyo kutoka kwenye umiliki wa wanachama na kuingia katika mfumo mpya wa ununuzi wa hisa.

Licha ya Kilomoni kupinga na baadaye kwenda mahakamani, wanachama walipitisha mabadiliko na kumwondoa kwenye Baraza la Wadhamini ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Alhaj Adam Mgoyi.

Mbali ya kuondolewa kwenye baraza hilo, Kilomoni alitakiwa kufuta kesi mahakamani pamoja na kujieleza na kama angeshindwa angefukuzwa uanachama moja kwa moja.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.