‘Yanga, Kagera ni kama Fainali Kombe la Dunia’

Bingwa - - HABARI -

NA WINFRIDA MTOI

MSHAMBULIAJI wa timu ya Kagera Sugar, Edward Christopher ‘Edo’, ameeleza jinsi walivyoipania mechi ya Yanga, huku akidai kuwa, wamepanga kucheza kwa kujitoa kama wapo kwenye Fainali za Kombe la Dunia.

Kesho Kagera wanatarajia kuwa wenyeji wa Yanga, ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, katika Uwanja wa Kaitaba, uliopo mjini Bukoba.

Katika mechi tano ambazo Kagera wamecheza, wamekusanya pointi mbili tu baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Ruvu Shooting na suluhu dhidi ya Majimaji 0-0, huku wakifungwa na Azam FC bao 1-0, Singida United 1-0 na Mbao FC 1-0.

Akizungumza na BINGWA jana, straika huyo alisema kila wanapokutana na timu kubwa mchezo hautabiriki, hivyo wanalazimika kucheza kulingana na hali watakayokutana nayo uwanjani.

Alisema kwa sasa kikosi chao kipo kwenye wakati mgumu, lakini furaha yao itarejea endapo watawafunga Yanga, ila matokeo yakiwa tofauti hali itazidi kuwa mbaya, hasa kwa mashabiki wao.

“Nakiri tumetetereka msimu huu, hivyo tunahitaji kushinda mechi dhidi ya Yanga ili kurudisha furaha yetu. Kikosi chetu si kibaya, bali hatuna bahati, ila tunawaahidi mashabiki wetu kuwa mechi ya Yanga tutacheza kama Fainali ya Kombe la Dunia,” alisema Edo.

Edo aliongeza kuwa, msimu uliopita Yanga waliwafunga mabao 6-2 katika mchezo wa awali na waliporudiana walifungwa 2-1, hivyo wana uwezo wa kupindua matokeo hayo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.