SIMBA: MTIBWA SUGAR HAITUUMIZI KICHWA

Bingwa - - HABARI -

NA SAADA SALIM

KOCHA Msaidizi wa timu ya Simba, Jackson Mayanja, amesema Mtibwa Sugar haiwauumizi kichwa kwa kuwa tayari wamepata dawa ya kuiua, katika mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba wanatarajia kucheza na Mtibwa Sugar kesho kutwa katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, ambapo kocha huyo raia wa Uganda amejigamba kuwa alipata dawa ya ushindi akiwa kwao.

Akizungumza na BINGWA jana, Mayanja alisema akiwa Uganda hakulala, kwani alikuwa akiendelea kufanyia kazi udhaifu walionao Mtibwa kupitia michezo waliyocheza.

Alisema anatarajia kukaa na bosi wake Mcameroon, Joseph Omog na kumpa ujanja wa kuifunga Mtibwa ili kuhakikisha wanaongeza pointi tatu nyingine baada ya kuifunga Stand United mabao 2-1 katika mchezo uliopita.

Mayanja aliongeza kuwa, kabla hajaondoka nchini alikiacha kikosi kikiwa vizuri, lakini alihakikisha anayafanyia kazi mapungufu ya Mtibwa ili washinde dhidi yao.

“Tunahitaji ushindi katika mchezo dhidi ya Mtibwa, naamini kila mchezaji anafahamu majukumu aliyopewa na benchi la ufundi,” alisema Mayanja.

Aidha, kocha huyo alieleza kuwa, pia wamewajenga kisaikolojia wachezaji wao ili wafanye vizuri katika mchezo unaowakabili.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.