Ndanda wapata kiburi uwanja wa nyumbani

Bingwa - - HABARI -

NA MAREGES NYAMAKA

NAHODHA wa timu ya Ndanda FC ya Mtwara, Rajab Zahir, amesema watatumia vema uwanja wao wa nyumbani wa Nangwanda Sijaona kuvuna pointi tatu dhidi ya Majimaji, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza na BINGWA jana, Zahir alisema watatumia mbinu zile zile walizotumia kuifunga Lipuli FC kuiangamiza Majimaji katika mchezo huo utakaopigwa kesho.

Zahir alisema kuwa, wachezaji wana morali ya hali ya juu kuhakikisha wanautumia vizuri uwanja wa nyumbani na kuibuka na pointi tatu ambazo zitasaidia kuwaweka nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

“Kikubwa tunatakiwa kutumia vema uwanja wetu na kupata matokeo ya ushindi, kwani tuna kila sababu ya kufanya hivyo, hasa kutokana na kikosi kuwa na wachezaji wenye viwango bora na uzoefu, hivyo Majimaji wajiandae kwa kipigo,” alisema.

Mchezo wa kesho utakuwa ni wa tatu kwa Ndanda kucheza katika uwanja wao wa nyumbani, ambapo Agosti 26, mwaka huu, walianza kwa kupata kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Azam, kabla ya kuzinduka na kuichapa Lipuli mabao 2-1.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.