Olimpiki Maalumu iwezeshwe kusaidia wenye ulemavu wa akili

Bingwa - - MAONI MTAZAMO KATUNI -

NI wazi kuwa michezo ni afya na ndiyo kaulimbiu inayotumika mara nyingi, katika mashindano na bonanza mbalimbali ya michezo yanapofanyika katika maeneo tofauti duniani.

Ili mtu aweze kuwa na afya njema jambo la kuzingatia ni kushiriki katika mazoezi, njia nzuri ya kufanya mazoezi ni kupitia michezo na ipo ya aina nyingi ambayo mtu yeyote anaweza kushiriki ili kuimarisha afya yake.

Tofauti na kuimarisha afya pia michezo inatumika kama burudani hasa katika kuhamasisha jambo katika jamii yoyote, mfano tumeona mara nyingi mashirika mengi yakitumia michezo kuifikishia jamii ujumbe husika.

Kamati ya Olimpiki Maalumu ‘Special Olympics Tanzania’, ni miongoni mwa taasisi zinazoamini katika michezo kuwa ni njia mojawapo ya kuwafanya watu kufurahia maisha na afya njema hasa kwa wale wenye ulemavu wa akili.

Special Olympics kwa wale wasiofahamu ni programu ya kimataifa ya michezo, kwa watu wenye ulemavu wa akili na ilianzishwa kwa lengo la kuwapa fursa watu hao kujifunza stadi za maisha na kukubalika katika jamii kupitia michezo.

Programu hizo za kuwawezesha watu wenye ulemavu wa akili kushiriki michezo, zipo 200 duniani kote na Tanzania ni miongoni mwao, pia wanaendesha mashindano yao kuanzia ngazi za mikoa, kitaifa na dunia.

Hata hivyo, kwa sehemu kubwa programu hizo zinategemea sana misaada ya watu binafsi katika kujiendesha na mara nyingi watu wanaofanya kazi na kamati za Special Olympics huwa wanajitolea.

Ifahamike kuwa ni kazi ngumu kuishawishi jamii kuamini au kukubali kuwa watu wenye ulemavu wa akili wana haki ya kushiriki katika michezo, ukizingatia wengi wamekuwa wakitengwa na kufichwa majumbani.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Special Olympics Tanzania, Michael Rays, Tanzania ina idadi ya watu wenye ulemavu wanaofikia 1,050,000 lakini wachezaji waliokuwa nao ni wachache kutokana na wengi kufungiwa majumbani.

Desemba mwaka huu, Tanzania inatarajia kufanya mashindano ya taifa ya michezo kwa watu wenye ulemavu wa akili, ambayo yatafanyika visiwani Zanzibar kwa kushirikisha wachezaji 500.

Kwa hali ilivyo na idadi ya wanamichezo wanaotarajiwa kushiriki, waandaaji ambao ni Special Olympics Tanzania, wanahitaji kusaidiwa kufanikisha mashindano hayo pamoja na kuendesha programu nyingine za kuwasaidia watu wenye ulemavu wa akili kupata haki ya kushiriki michezo hiyo kwani moja ya faida za kushiriki ni kuwasaidia kutoka katika hali hiyo.

Tayari kamati hiyo imeweka wazi kiasi cha fedha shilingi milioni 75.5, ili kufanikisha mashindano hayo ambayo lengo ni kupata wachezaji wa kwenda kushiriki michuano ya dunia nchini Abu Dhabi mwaka 2019.

Ni dhahiri kuwa michezo ya watu wenye ulemavu imekuwa ikisahaulika, hivyo kuifanya irudi nyuma au kufa kabisa kutokana na kukosa wadhamini ambao wengi wanakimbilia kwenye soka.

Naamini kama programu za michezo ya watu wenye ulemavu wa akili zitawezeshwa, mashindano yatakuwa yanafanyika mengi, hali itakayobadilisha mitazamo ya jamii juu ya watu hao.

Kama fedha wanazohitaji zitapatikana na mashindano yakafanyika katika hali ya kuvutia bila changamoto nyingi, itawahamasisha wazazi wenye tabia ya kufungia watoto wenye ulemavu wa akili kuwaachia kirahisi kushiriki michezo.

Nimeshuhudia baadhi ya watoto wa aina hiyo wanaopewa nafasi ya kushiriki michezo na kujumuika na watu wengine, wakichangamka tofauti na wale wanaokaa nyumbani.

Wazazi, kampuni na mashirika mengine yenye uwezo wa kusaidia kufanikisha mashindano haya wajitokeze kuwasaidia Special Olympics, ili kuwaunga mkono katika harakati zao za kuhakikisha walemavu wa akili wanapata haki ya kucheza na kufurahi.

Desemba mwaka huu, Tanzania inatarajia kufanya mashindano ya taifa ya michezo kwa watu wenye ulemavu wa akili, ambayo yatafanyika visiwani Zanzibar kwa kushirikisha wachezaji 500.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.