BODI YA LIGI ITAKAYOCHAGULIWA ISHUGHULIKIE KERO HIZI

Bingwa - - MAONI MTAZAMO KATUNI -

BODI ya Ligi inatarajia kupata viongozi wapya baada ya uchaguzi uliopangwa kufanyika Jumapili, chini ya Usimamizi wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), inayoongozwa na mwenyekiti wake, Revocatus Kuuli.

Kampeni za wagombea za kunadi sera kwa wapiga kura zilianza Jumapili iliyopita, ambapo katika nafasi ya uenyekiti inawaniwa na watu wawili, ambao ni Clement Sanga na Hamad Yahya, anayetetea nafasi yake.

Uchaguzi wa Bodi ya Ligi unakuja kukiwa na changamoto lukuki, hasa katika Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.

Baadhi ya changamoto hizo, ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikilalamikiwa na baadhi ya klabu zinazoshiriki katika ligi hizo, ni ubovu wa viwanja, upangaji mbaya wa ratiba na ucheleweshaji wa kutoa uamuzi kwa baadhi ya kesi zinazofikishwa mbele ya bodi hiyo.

Sisi BINGWA tunaomba viongozi watakaochaguliwa kuzifanyia kazi kero hizo, ambazo kwa kiasi fulani zimekuwa zikichangia kurudisha nyuma maendeleo ya soka letu.

Tukianza na kero ya viwanja, BINGWA tunaona viwanja vingi nchini ambavyo vinatumika kwa ajili ya ligi hizo havikidhi matakwa ya Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa, kutokana na kutofanyiwa matengenezo ya maana, licha ya wamiliki wake kuingiza kiasi kikubwa cha fedha kitokanacho na mgawo wa mapato ya mechi.

Tuna imani viongozi watakaochaguliwa watakaa meza moja na wamiliki wa viwanja hivyo, ambavyo vingi vinamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili kuangalia namna ya kuviboresha.

Katika changamoto ya upangaji ratiba, tunawashauri viongozi hao wapya watakaoingia madarakani na watakaofanikiwa kutetea nafasi zao kuangalia jinsi ya kulifanyia kazi.

Ushauri huu unatokana na kwamba, baadhi ya klabu hazina fedha za kutosha, hivyo wanatakiwa kuangalia jinsi ya kuzipa unafuu katika safari zao za kucheza mechi za ugenini na kama tatizo halitakuwapo, huenda ratiba hiyo ikawa na tija na kuzitua mzigo wa gharama ambazo zimekuwa zikilazimika kuingia.

Kwa upande wa uchelewaji wa kutoa uamuzi kwa baadhi ya kesi, BINGWA tunaona utakuwa ni muda mwafaka wa kufanyika mabadiliko kwa baadhi ya kanuni zinazoendesha bodi hiyo.

Tunaona hivyo kutokana na kuwa, kwa sasa bodi hiyo haina meno ya kuweza kushughulikia kesi bila kutegemea kamati nyingine.

Hilo ni jambo ambalo halipingiki, kutokana na kwamba bodi ya sasa inaruhusiwa kumsimamisha mtu tu na huku ikisubiri awajibishwe na kamati husika.

Tuna imani kama jambo hilo litafanikiwa litaipa uhuru zaidi bodi hiyo kutoa maamuzi na pia litapunguza baadhi ya gharama ambazo imekuwa ikiingia za kuwalipia gharama wajumbe wa baadhi ya kamati ili vikao vyao viweze kutoa uamuzi kwa wakati na pia itapunguza malalamiko hayo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.