ALLIANCE GIRLS YATINGA LIGI KUU WANAWAKE

Bingwa - - STORI ZA KITAA -

NA MASYENENE DAMIAN, MWANZA

USHINDI wa mabao 6-0 dhidi ya Allan ya Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri, juzi umewapa tiketi mabingwa wa soka la wanawake Mkoa wa Mwanza Alliance Girls, kucheza ligi kuu ya wanawake Tanzania Bara msimu wa 2017/18.

Mchezo huo ndio ulikuwa unaamua hatima ya timu hiyo kucheza ligi kuu ya wanawake, ambapo walikuwa wanahitaji alama moja tu kukata tiketi hiyo, hivyo ushindi huo mnono umewafanya kuwa mabingwa wa kituo cha Dodoma, chenye timu tano za Unyanyembe ya Tabora, Allan ya Dodoma, Njombe, Songwe na Alliance wenyewe.

Alliance wametangazwa mabingwa baada ya kushinda mechi zake nne na kufikisha pointi 12, ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kwenye kundi hilo, wakiwa wamefunga mabao 26 na kufungwa bao moja peke yake.

Mchezo huo, uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu na benchi la ufundi na viongozi wa timu hiyo kwenda ligi kuu, ulipigwa juzi jioni dhidi ya wenyeji Allan, ambapo walishinda mabao 6-0, yakifungwa na nyota wake, Janeth Maturanga aliyeweka mabao mawili, mengine yakifungwa na Esther Mabanza, Sharifa Hamidu, Rahabu Joshua na Anna Baltazari, aliyekamilisha karamu hiyo ya mabao.

Mabao hayo mawili yanamfanya mshambuliaji Janeth, kuendelea kung’ara zaidi baada ya kufikisha mabao 13 kwenye michezo mitatu aliyocheza, hivyo kumfanya atangazwe mfungaji bora wa kundi hilo.

Baada ya ushindi huo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ezekiel Chobanka, aliliambia BINGWA kwamba, hana mpango wa kufanya usajili wa kukiongezea makali kikosi chake kabla ya kuanza kwa michezo ya ligi kuu ya wanawake, kwa sababu kituo hicho kina wachezaji wenye vipaji wa kutosha.

“Tunashukuru kwa mafanikio haya na tunajipanga kufanya vizuri kwasababu kuna mapungufu madogomadogo tuliyabaini, lazima tuyafanyie kazi ili tuwe vizuri zaidi, hatuna mpango wa kusajili kwasababu hii ni ‘academy’, kuna wachezaji wengi hatujawatumia, hivyo tunayo hazina ya kutosha ya vipaji,” alisema Chobanka.

Katika mchezo wa kwanza, timu hiyo ilishinda bao 1-0 dhidi ya Njombe, baadaye ikaizamisha Songwe mabao 11-0, kabla ya kuichapa Unyanyembe mabao 8-1 na kumaliza michezo yake kwa kuivurumisha kwa mabao 6-0 wenyeji Allan. Kikosi hicho kinatarajia kurejea kesho jijini Mwanza kuendelea na kambi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.