TPB yazindua promosheni mpya

Bingwa - - STORI ZA KITAA -

NA MWANDISHI WETU

BENKI ya Posta (TPB) imezindua promosheni ya huduma ya Western Union, ambayo itawawezesha watumiaji wa huduma ya kifedha kushinda fedha, simu za kisasa za mkononi na kompyuta mpakato (laptop).

Akizungumza jijini jana, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Ukuaji wa Biashara wa TPB, Frank Mushi, alisema wameamua kuanzisha shindano hilo kama kuwazawadia wateja wake katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.

Mushi alisema washindi wanaweza kupata kiasi cha fedha ambacho kitawawezesha kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka, kwani watumiaji wawili wa Western Union wanaweza kushinda zawadi hadi kufikia Sh milioni tatu.

Alisema mbali na benki hiyo, promosheni hiyo pia itawashirikisha washirika wao kama Shirika la Posta Tanzania (TPC), Benki ya DCB, Benki ya Azania, Benki ya Wakulima ya Kagera, Benki ya Mwanga, Benki ya Amana, Benki ya Uchumi, Benki ya Maendeleo, Benki ya Njombe, Benki ya Mufindi na Benki ya Kilimanjaro.

“Promosheni tunayozindua leo ni ya miezi mitatu, ambayo itakwisha mwezi Januari, mwakani na inakusudia kuwashukuru na kujiweka karibu zaidi na wateja wetu ambao wanaitumia huduma hii ya Western Union.

“Droo ya kwanza itafanyika katikati ya mwezi ujao, ambayo itatoa washindi awali na kila mmoja atapata Laptop na washingi watano kila mmoja atapata simu za kisasa za mkononi,” alisema Mushi.

Alisema kuwa, droo ya pili itafanyika katikati ya Desemba, mwaka huu na Januari 2018.

Utoaji wa zawadi za washindi utafanyika kwenye tawi husika ambako mteja ametuma au kupokea fedha na kujaza kuponi ya kushiriki kwenye promosheni.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.