HAYA NI MAAJABU MENGINE YA MESSI

Bingwa - - TOP TEN TAKWIMU -

LONDON, England

JUMANNE ya wiki hii, Lionel Messi, aliishangaza dunia kwa ‘hat trick’ yake iliyoipeleka timu ya Taifa ya Argentina kwenye fainali za Kombe la Dunia za mwakani nchini Urusi.

Kama si mabao hayo matatu ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 katika mchezo dhidi ya Ecuador, basi Argentina ingezikosa fainali hizo zitakazoanza Juni nchini Urusi.

Messi alipachika bao la kwanza katika dakika ya 12 likiwa ni la kusawazisha, akaweka lingine katika dakika ya 20, kabla ya kumaliza kazi katika dakika ya 62.

Hata hivyo, hebu chungulia maajabu mengi aliyowahi kuyafanya ‘mnyama’ huyo katika maisha yake ya soka.

‘Hat-trick’ ya Clasico (Machi 2007)

Kilichowashangaza wengi katika mtanange huo ni kwamba, kwanza alikuwa na umri wa miaka 19. Pia, ilikuwa ni Clasico yake ya tatu tu.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Camp Nou, Messi aliwaacha hoi Madrid akifunga mara tatu na kuisaidia Barca kuambulia sare ya mabao 3-3.

Bao la mwisho alifunga zikiwa zimebaki dakika 87 huku Barca wakiwa wamebaki 10 uwanjani.

Mabao matano (Machi 2012)

Messi alilifanya balaa hilo katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati Barcelona walipokutana na Bayer Leverkusen ya Bundesliga.

Kwa mauaji hayo, Messi alitajwa kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao matano katika mchezo mmoja wa michuano hiyo.

Akiwa na umri wa miaka 24 kipindi hicho, Muargentina huyo alifunga mara mbili kabla ya timu hizo kwenda mapumziko, kabla ya kumalizia ‘hat trick’ katika kipindi cha pili.

Mabao hayo yaliiwezesha Barca kutinga robo fainali kwa kishindo, ikiwa na jumla ya mabao 7-1.

Alivyoiua Madrid (Aprili 2017)

Ulikuwa ni mchezo ambao Barca walitakiwa kuichapa Madrid ili kufufua matumaini ya ubingwa wa La Liga.

Baada ya kuitanguliza Barca kwa kuwalamba chenga mabeki wawili wa Madrid, timu hizo zilikuwa sare ya mabao 2-2 hadi zikiwa zimebaki sekunde chache kabla ya kumalizika kwa mchezo huo.

Shuti lake la mwisho katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Bernabeu, ndilo lililobadili matokeo na kuipa Barca ushindi wa mabao 3-2. Yalikuwa ni maajabu ambayo wachezaji na mashabiki wa Madrid walibaki kujiuliza ilikuwaje Messi akawaharibia mwishoni kabisa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.