JEURI YA MOURINHO IKO HAPA

Bingwa - - MBELE -

ZIMEKUWA ni wiki mbili za mikiki mikiki ya mechi za kufuzu kushiriki michuano ya Kombe la Dunia. Vicheko, vilio na kila aina ya hisia ilionekana kabla ya kufikia mwishoni mwa wiki hii. Mataifa mbalimbali yakifurahia kwenda Urusi na mengine yakilia kwa kuikosa nafasi, yote ni matokeo kwenye mashindano ambayo kwa namna moja ama nyingine, kwetu sie wa kubeti ni chanzo cha kutunisha pochi.

Wikiendi hii kuna mechi kali mno za ligi mbalimbali kwa upande wa klabu na kama kawaida, Mzee wa Kubeti nakuambia usikubali kuuchana mkeka wako kwa kuacha kupitia dondoo hizi za leo.

LIVERPOOL v MAN UNITED

United watacheza mechi ya kwanza yenye upinzani haswa Premier League dhidi ya Liver, ambayo imeanza kwa kasi ndogo, tofauti na mategemeo ya wengi na kesho watamkosa Mane, anayesumbuliwa na msuli wa paja.

Kabla ya kupisha mapumziko, matokeo ya mwisho ya Liver yalikuwa ni sare, ukiwa ni mwendelezo wa mechi saba (ushindi mmoja), kiujumla msimu huu wameshinda mechi tano, sare tano na kufungwa mbili, kiwango dhaifu kilichosababisha watolewe Carabao Cup, nafasi yao kwenye makundi Champions League ikiwa si nzuri sana. Kinachowaangusha ni safu nyanya ya ulinzi, iliyoruhusu mabao 20 kwenye mechi 12, huu ni udhaifu ambao huenda ukawafaidisha United kesho.

United wamefunga mabao 32 kwenye mechi 10 za michuano yote msimu huu, hakuna mechi waliyomaliza bila bao, huku mfungaji wao hatari akiwa ni Romelu Lukaku. Kwa kuyaangalia matokeo matano ya mwisho ya hizi timu, hii ni mechi ngumu kwa pande zote (Liver haijafungwa na United kwenye mechi tatu za mwisho). United licha ya kwamba wana mabeki wazuri, walifungwa mabao mawili na Stoke, ambayo si timu inayotisha kiushambuliaji, tofauti na Liver, yenye mabao 12 kwenye mechi zao tano za mwisho.

Utabiri: Liverpool 2-2 Man Utd

JUVENTUS v LAZIO

Wikiendi hii imetawaliwa mno na mechi kali za Serie A, tukianza na hii ya Juventus dhidi ya Lazio. Mara ya mwisho kukutana wakali hawa, Lazio iliichapa Juve bao 3-2 kwenye fainali ya Supercoppa.

Juve wataingia kwenye mchezo huo na nia moja ya kushinda ili kuwafukuzia kwa kasi vinara wa ligi, Napoli. Na wanaonekana kuwa vizuri sana kwa msaada mkubwa, lakini wa straika Paulo Dybala, mwenye mabao 10 ndani ya mechi saba, na kwa sababu hii Juve wana nafasi ya kuibuka na ushindi kesho, kwani ndani ya mechi 11 walizokutana na Lazio, wameshinda 10.

Utabiri: Juventus 2-0 Lazio ROMA v NAPOLI

Mechi nyingine kali ya Serie A hii hapa, moja ya mechi kubwa Italia. Nani kuibuka mbabe wa mji kesho? Ni vinara wa ligi, Napoli ama Roma.

Kwa misimu miwili, Napoli wanaonekana kulipania sana taji la Serie A, lakini bado wana safari ndefu ya kutimiza ndoto yao na hili ni moja ya jaribio zito kwao msimu huu, katika pambano la mwisho baina yao msimu uliopita, Napoli waliichapa Roma, na hata wiki chache zilizopita waliwapiga ndugu zao, Lazio mabao 4-1 kwenye dimba la Olimpico, wakionesha uimara kwenye safu ya ulinzi sambamba na makali katika kushambulia. Ni wazi Napoli wapo kwenye kiwango bora msimu huu.

Roma nao wamepata matokeo mazuri pia msimu huu, ingawa hayajawa ya kuridhisha kama wapinzani wao, Napoli, ambao wamekuwa wakitegemea sana makali ya wapachika mabao wao, Dries Mertens, Lorenzo Insigne na Jose Callejon, walioisaidia timu yao kushinda mechi 11 kwa wastani wa bao tatu tatu. Hatari! Utabiri: Roma 1-3 Napoli

INTER V MILAN

Wakati Milan wanasajili kwa fujo, watu walidhani ingeanza kwa kasi kubwa sana, lakini tofauti na matarajio, ni wapinzani wao wa jadi, Inter, walioanza vizuri, licha ya kutosajili sana, kwani kikosi chao kimetulia na kutosumbuliwa na presha kama wenzao.

Katika mechi dhidi ya timu zinazojua kukaba haswa, Milan wameshindwa kufurukuta kabisa, tayari wamepokea vichapo vya 4-1 kwa Lazio, 2-0 kwa Sampdoria na Roma, inamaanisha hawapo tayari kwa vita na Jumapili watawezaje kujitetea mbele ya wapinzani wao wa jadi, Inter?

Wapinzani wao hao walikuwa wakisumbuliwa sana na changamoto kama yao, lakini wameonekana kutulia sasa na wameweza kushinda mechi sita kati ya saba za mwisho msimu huu na ndio wenye dalili zote za kushinda wakiwa kwenye dimba la Giusseppe Meazza.

Utabiri: Inter 2-1 Milan

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.