Uteuzi wanaowania Ballon d’Or ulivyodanganya mashabiki

Bingwa - - IJUMAA - HASSAN DAUDI 0746 252856

KABLA ya kuingia kwenye mada ya leo, acha nigusie kidogo kile kilichofanywa na staa Lionel Messi Jumatano ya wiki hii, ambacho kwa hakika kimezua gumzo kwenye ulimwengu wa soka. Ni ngumu kupotezea maajabu ya Messi juzi usiku.

Kama ulipitwa, Argentina walikuwa wanacheza na Ecuador, ukiwa ni mchezo uliokuwa na maana kubwa kwa Messi na taifa lake hilo la Kusini mwa Bara la Amerika.

Endapo Argentina wangepoteza, basi wangeitazama michuano hiyo ya Kombe la Dunia kupitia vituo vya televisheni na si ushiriki wa moja kwa moja.

Katika hali iliyowashangaza wengi na kuibua shangwe kwa mashabiki wa Argentina, Messi anatupia ‘hat trick’ katika ushindi wa mabao 3-1, matokeo ambayo yamewapeleka moja kwa moja Argentina kwenye fainali hizo ambazo zitakuwa za 21.

Kwa umri wake wa miaka 30, ikionekana wazi kuwa ni ngumu kwa kipindi kilichobaki kwenye maisha yake ya soka kuipa Argentina taji la kombe la dunia, huenda hiyo itabaki kuwa zawadi kubwa kuitoa kwa taifa lake.

Ni wazi nyota huyo amewafunga mdomo wakosoaji wake ambao wamekuwa wakisema huwa hajitoi kulipigania taifa lake, tofauti na anapokuwa na klabu yake ya Barcelona.

Hata hivyo, kabla ya hilo la maajabu ya Messi na Argentina, kulikuwa na taarifa ya wanasoka 30 waliotajwa na jarida la France Football kuwania tuzo ya Ballon d’Or.

Ukweli ni kwamba, binafsi nilibaki na maswali mengi baada ya kuiona orodha hiyo na hata kujikuta nikitilia shaka umakini wa jarida hilo katika kumsaka mshindi.

Haikushangaza kuyaona majina kama Gianluigi Buffon, Paulo Dybala, Antonie Griezmann, Eden Hazard, Lionel Messi, Neymar, Cristiano Ronaldo na Luis Suarez.

Lakini je, France Football walitumia vigezo gani kutudanganya kuwa Mats Hummels, Sadio Mane, Philippe Coutinho, Luis Suarez na Karim Benzema wanastahili kuwamo?

Kwa upande wa Hummels, nini alichokifanya zaidi ya klabu yake ya Bayern Munich kubeba taji la Bundesliga na kuitoa Arsenal katika Ligi ya Mabingwa. Hivi, France Footall wanatuaminisha kuwa Hummels alikuwa bora kuliko Javi Martinez na Philipp Lahm?

Ilishangaza kidogo kumuona Hummels akiwania tuzo ya Ballon d’Or, huku Carvajal, aliyeipa Real Madrid taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akipotezewa?

Pia, France Football ilitudanganya kumuweka Mane kwenye orodha ya wanasoka 30 wanaotakiwa kuibeba Ballon d’or. Msenegal huyo amekuwa silaha ya Liverpool kwa muda sasa, lakini bado si mchezaji aliyetakiwa kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.

Kwa kuwa mshindi wa Ballon d’Or hupimwa kwa mafanikio yake katika ngazi ya timu ya taifa na klabu, amesema France Football wametudanganya kwa kitendo chao cha kuliweka jina la Mane kwenye orodha hiyo ya wanasoka 30.

Ndiyo, Mane ameipa taji gani Liver? Msimu uliopita, kikosi chake kiliondoshwa na ‘vibonde’ Wolverhampton katika Kombe la FA na hata kwenye Kombe la Ligi walichapwa na Southampton.

Kwa Coutinho, pia ni ajabu kuliona jina lake kwenye mbio za kuiwania Ballon d’Or. Ni kweli Mbrazil huyo alikuwa bora msimu uliopita kuliko wengine Ligi Kuu England? Hapana.

Ni kama ilivyotokea kwa Suarez tu, ambaye huenda jina lake lingestahili kuwamo endapo mshindi wa tuzo hiyo angekuwa anapatikana kwa mafanikio ya miaka mingi iliyopita.

Msimu uliopita alifunikwa na kivuli cha mastaa Neymar na Messi. Katika mabao yake 25, ni mawili pekee yaliyokuwa ya kuiokoa Barca na kipigo.

Vipi kuhusu Benzema? Ni kweli alistahili kutajwa kwenye orodha ya wanaoweza kuibeba Ballon d’Or? Kama nilivyosema hapo awali, huo ni uongo mwingine wa jarida la France Football. Benzema hakuwa na nafasi hata kidogo.

Nini alichokifanya Mfaransa huyo na hata kupata nafasi? Inashangaza na kuacha maswali mengi yasiyo na majibu. Tangu kuanza kwa mwaka huu, Benzema amepachika mabao 10 na ni mawili tu aliyofunga, wakati Madrid wakiwa kwenye hatari ya kupoteza mchezo.

Hapo ndipo unapojiuliza, ni kigezo gani kilichotumika kumpa nafasi Benzema na kumuacha kiungo wa Manchester United, Paul Pogba?

Inafikirisha zaidi pale unapogundua kuwa, kwa muda mrefu sasa, Benzema amekuwa hapati nafasi hata kwenye kikosi cha timu yake ya Taifa ya Ufaransa, kinachonolewa na kocha Didier Deschamps.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.