Cotto kustaafu baada ya kuzipiga na Ali

Bingwa - - HABARI - NEW YORK, Marekani

BINGWA wa zamani wa dunia mara sita wa ngumi, Miguel Cotto, anatarajiwa kuachana na mchezo huo, baada ya pambano lake la uzani wa light-middle dhidi ya Sadam Ali, ambalo limepangwa kufanyika Desemba 2, mwaka huu.

Bondia huyo mwenye umri wa miaka 36 ambaye amewahi kutwaa mataji manne katika uzani tofauti, anatarajia kutetea taji lake la WBO kwa mara ya mwisho katika pambano hilo ambalo litafanyika jijini New York katika ukumbi wa Madison Square Garden.

Hadi sasa Cotto ameshashinda mapambano 41 kati ya 46 huku mabondia; Floyd Mayweather, Manny Pacquiao na Saul 'Canelo' Alvarez, wakiwa kati ya walioshiriki katika vipigo vitano alivyoviambulia.

Bingwa huyo pia wa zamani wa dunia katika ngumi za uzani wa light-welter na welter, alifanikiwa kutetea taji lake la WBO katika uzani wa light-middle baada ya kumshinda Mjapan, Yoshihiro Kamegai, likiwa limeonekana kuwa ni pambano lake la mwisho katika mchezo huo.

"Nina furaha kubwa kwa kurejea tena ulingoni katika pambano langu ambalo sasa litakuwa ni la mwisho," alisema Cotto.

"Nimekuwa nikijituma sana hadi kufikia kiwango hiki. Nimekuwa nikizingatia mazoezi yangu chini ya mkufunzi wangu Freddie Roach, hivyo na sasa tutajituma ili Desemba 2 tuweze kupata ushindi mnono,” aliongeza bondia huyo.

Kwa upande wake Mmarekani, Ali ameshashinda mapambano 25 kati ya 26.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.