ZAINAB MREKWA:

SISHABIKII SIMBA WALA YANGA, DON BOSCO NDIO MPANGO MZIMA

Bingwa - - MAKALA - NA SHARIFA MMASI

UKIBAHATIKA kukutana na wachezaji wenye mapenzi na michezo wanayoipenda na kuwauliza maswali kuhusu upande mwingine, tegemea majibu yao yatakuwa tofauti na ulivyotarajia. Miongoni mwa wachezaji hao ni Zainab Mrekwa (22), anayecheza mpira wa kikapu katika timu ya Don Bosco Lioness, yenye makazi yake Upanga, jijini Dar es Salaam. Mrekwa, anayevaa jezi namba 11, ni miongoni mwa wachezaji wa kike waliokuwa gumzo katika michuano ya Ligi ya Kikapu ya Mkoa wa Dar es Salaam (RBA) mwishoni mwa mwezi uliopita, kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, jijini. Mbali na kutajwa kwa umahiri wake awapo uwanjani, pia anasifika kwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wenzake kuishambulia timu pinzani hadi ikafanikiwa kushika nafasi ya pili wakiwa nyuma ya mahasimu wao, Vijana Queens, walionyakua taji hilo baada ya kuibuka na ushindi wa vikapu 72 dhidi ya 69 katika mchezo wa fainali. BINGWA lilifanya mahojiano na Mrekwa, kwa lengo la kutaka kufahamu mengi kuhusu maisha yake ndani na nje ya mpira wa kikapu. Mrekwa anasema kuwa, 2012 ndio mwaka rasmi aliojikita katika mchezo huo, akiwa na klabu ya Don Bosco, ambayo aliitumikia kwa muda wa mwaka mmoja, kabla ya kupumzika kutokana na kukabiliwa na masomo ya kidato cha nne. “Nilitokea kuvutiwa na mchezo wa kikapu na hivyo mwaka 2012 nikaamua kujikita rasmi nikiwa na Don Bosco, ingawa niliitumikia timu hiyo kwa muda wa mwaka mmoja tu kutokana na kukabiliwa na masomo,” anasema nyota huyo.

“Lakini kama unavyofahamu, ukichanganya mambo mawili kwa wakati mmoja haifai, wakati huo nilihitaji kufanya vyema kwenye mitihani yangu ya kidato cha nne, ndiyo maana ilinilazimu niache kikapu hadi nilipomaliza mitihani yangu,” Mrekwa anabainisha zaidi.

Anasema baada ya kumaliza masomo yake, ndipo sasa akaamua kurejea kwenye kikosi chake cha Don Bosco Lioness ili kuhakikisha anakitumikia akiwa na akili moja bila kuwa na mawazo mengine zaidi ya mchezo huo.

Anasema jambo hilo ndilo amelidhihirisha hadi sasa na mafanikio yake yameshaanza kuonekana.

Akizungumzia kuhusu ushabiki wa michezo mingine, Mrekwa anasema, katika maisha yake hakuwahi kushabikia timu yoyote ya soka, tofauti na ilivyo kwa wachezaji wengine wa kikapu.

“Mbali na mchezo wa kikapu, sijawahi kuwa na mapenzi na mpira wa soka, hususan hizi timu za Simba na Yanga.

“Mimi na Don Bosco tu, kwani naamini klabu hiyo imenitoa mbali na itanifikisha mbali kimaisha, ndiyo maana natumia muda mwingi kupambana kimazoezi ili kuhakikisha nafanya vyema uwanjani kwa ajili ya kuiletea sifa na mafanikio,” anasema nyota huyo. Anasema anaipenda sana timu hiyo, kutokana na kwamba ndiyo imemsaidia katika mambo mengi, likiwamo la kumnyanyua kimasomo kwa kumlipia ada pindi alipokuwa akihitaji msaada kama huo.

“Sitaki kuwa mnafiki, mpira wa kikapu umenifikisha mbali sana, kwanza nimeweza kufahamiana na watu ambao sikutarajia kukutana nao katika maisha yangu,” anasema nyota huyo.

“Nimeshatembea nchi nyingi sana kupitia huu mchezo, mbali na hilo, uongozi wa klabu ya Don Bosco unanisaidia kulipa ada ya shule pale ninapokwama na mambo mbalimbali,” anaongeza staa huyo.

Akizungumzia changamoto anazokumbana nazo kama mchezaji wa kike, anasema mpangilio wa mechi za usiku kwake na baadhi ya wanawake wengine limekuwa tatizo kubwa.

“Moja ya changamoto inayonikabili mimi ni muda wa kurudi nyumbani, wakati mwingine mechi tunapangiwa kucheza usiku, au inaanza jioni na kumalizika usiku, ninaporudi nyumbani mzazi hakuelewi.

“Ikitokea umemwelewesha na kukuelewa, basi kwanza utasemwa mpaka unaumia, ndipo wazazi wakuelewe, hii ni changamoto kubwa kwangu, nafikiri hata kwa wachezaji wengine wa kike ambao wapo chini ya wazazi wenye kujua maadili,” anasema Mrekwa.

“Mimi na Don Bosco tu, kwani naamini klabu hiyo imenitoa mbali na itanifikisha mbali kimaisha, ndiyo maana natumia muda mwingi kupambana kimazoezi ili kuhakikisha nafanya vyema uwanjani kwa ajili ya kuiletea sifa na mafanikio,”

DonBosco Lioness

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.