SAFARI YA JASHO NA DAMU YA UGANDA NA MISRI INATUHUSU TANZANIA PIA

Bingwa - - UCHAMBUZI -

HISTORIA ya vitu vingi katika uso wa dunia inasemekana ilianzia katika ardhi ya Farao. Ardhi ambayo Musa alitumwa kuwaokoa wana wa Israel waliokuwa utumwani kwa zaidi ya miaka 100.

Ni historia ya kipekee ambayo inaendelea kuishi katika vitabu au maandiko ya dini kuhusu utawala wa Farao wa Misri. Alikuwa na nguvu ya utawala, pamoja na jeshi lililotii kila alichowaamuru.

Misri ni nchi ya kipekee sana katika Bara la Afrika, bado hata historia kuhusu namba inasemekana zilianzia huko, pia hata ubunifu wa kalenda na mambo mengine mengi yalianza katika uso wa ardhi hiyo ya Farao mwenye mamlaka.

Hata katika historia ya soka la Afrika, nchi hiyo inakamata usukani ikiwa timu iliyoshinda makombe mengi ya Afcon zaidi ya timu nyingine yoyote, wakiwa wameshinda kombe hilo mara saba.

Nadhani kila mmoja ameiona safari yao waliyopitia kuelekea Kombe la Dunia litakalofanyika nchini Urusi mwaka 2018. Hakika walistahili kuvunja mwiko huo uliowakwamisha kwenda kushiriki kwenye fainali hizo tangu mwaka 1990.

Mwaka ambao hapa nchini Tanzania, ilikuwa chini ya Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi. Miaka ambayo jina la mzee wa ruksa lilishika kila kona ya nchi hii.

Kwa aina ya wachezaji wa Misri wakati ule ilifanya watu washangae, kwanini walikuwa wanakosa kushiriki Kombe la Dunia? Walikuwa na kocha mzuri pamoja na wachezaji wenye vipaji vikubwa.

Kila mara waliishia njiani, lakini lilipokuja suala la Kombe la Mataifa ya Afrika walionekana kuwa wakali sana, kiasi cha kushinda kombe hilo mara nyingi zaidi ya taifa lolote barani Afrika.

Karibu asilimia 90 wachezaji wa Misri walikuwa wanacheza ligi ya nyumbani wakati ule. Licha ya kuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuchezea kwenye ligi za Ulaya, kwao ilionekana ni fahari kubwa kuwa shujaa ambaye unatokea nyumbani moja kwa moja.

Kipaji cha Mohamed Aboutrika kiliishia kucheza Tersana na Al Ahly tu, huku siku za uzee wake kabla hajastaafu aliishia kutolewa kwa mkopo kwenda timu ya Baniyas iliyopo katika Falme za Kiarabu (UAE).

Huyo ni moja ya wachezaji bora wa muda wote wa Misri ambaye kwa hakika alifanana na Zinedine Zidane kwa kila alichokifanya uwanjani, lakini aliishia kucheza Afrika tu.

Naamini kufuzu kwa Misri kwenye fainali hizi za Kombe la Dunia kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na wachezaji wao wengi kucheza ligi za Ulaya.

Ukianzia kwa nyota wa timu hiyo, Mohammed Salah, anayekipiga Liverpool, pia kuna Mohammed Elneny kutoka Arsenal, Ramadan Sobhi wa Stoke City, Ahmed Elmohamady anayekipiga Aston Villa, Sam Morsy kutoka Wigan, RhamiJasin Ghandour anakipiga katika timu ya Vfl Wolfburg na nyota wengine wengi wanaokipiga nje ya ligi yao ya nyumbani.

Ukiacha nchi yao kuvunja mwiko wa kutoshiriki michuano hiyo tangu mwaka 1990, pia ni fahari kwa wachezaji hao wanaocheza kwenye klabu za Ulaya.

Mbegu hizo za mafanikio yao, walizipanda katika ardhi ya kuamini soka la vijana linaweza kuwafikisha mbali, kwa asilimia kubwa wachezaji wanaovaa jezi ya taifa hilo ni wale waliowakuza kwenye shule za mpira. Hivi sasa nchi hiyo ina wachezaji wengi chipukizi wanalelewa katika shule za vipaji za timu za Ulaya, hiyo ndiyo njia pekee iliyozaa matunda kutoka kwenye mbegu hizo.

Ufahari uliyopo Misri, upo pia Uganda. Hawa ni majirani zetu ambao miezi michache iliyopita tulizindua nao ujenzi wa bomba la mafuta pale Mkoa wa Tanga.

Maendeleo haya tunayofanya nao kwenye jamii, kwa upande wa pili wametuacha mbali katika ramani ya mpira wa miguu. Thamani ya vipaji vyao inaonekana sasa.

Binafsi sikuhitaji wafuzu kwenye fainali za Kombe la Dunia ila nilihitaji wapate kujifunza jinsi ya kufuzu michuano hiyo. Naamini wamejifunza mambo mengi, wakati mwingine watakuja wakiwa kamili zaidi.

Awali walifanikiwa kufuzu Michuano ya Mataifa ya Afrika baada ya kipindi kirefu kupita. Lakini walianza kwa kusuasua, mwisho wa siku walienda Gabon kwenye fainali hizo.

Uganda ni majirani zetu ambao kijiografia tumetenganishwa nao na Ziwa Victoria. Basi kama tunavyoshirikiana nao kwenye mambo mengine ya maendeleo tusione haya kuwafuata na kujifunza kuhusu safari yao ya mafanikio ya soka la nchi yao. Itatusaidia kutoka tulipo na naamini itakuwa njia nzuri ya mafanikio ya mpira wetu uliojaa ubabaishaji.

Misri na Uganda wametumia nguvu kubwa kuendeleza soka la vijana ambalo hapa Tanzania, bado tunaona miujiza. Mafanikio ya mpira wetu yapo kwa vijana, tutumie nguvu kubwa kuwekeza japo kwa wengine inaweza kuwa shida kutokana na timu zao nyingi kuangalia matokeo pekee.

Nje ya soka la vijana, basi tujitahidi kuuza wachezaji wetu nyota ligi zilizopiga hatua kama ilivyotokea hivi karibuni kwa Simon Msuva na Abdi Banda. Hakuna uchawi kwenye maendeleo ya soka zaidi ya kujikita katika soka la vijana. Bila hilo itakuwa ndoto kwetu kufika sehemu

tunayohitaji.

Kila mara waliishia njiani, lakini lilipokuja suala la Kombe la Mataifa ya Afrika walionekana kuwa wakali sana, kiasi cha kushinda kombe..

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.