NILISHAKUFA

Bingwa - - HADITHI MALAVIDAVI - Ilipoishia Askari walikuwa wakifanya ukaguzi mkubwa sana pale kituoni hasa kwa mabasi yanayoondoka nje ya Uganda. facebook: feman cross emanfisima@yahoo.com

SASA ENDELEA

Kila mtu alikaguliwa yeye na mizigo aliyokuwa ameibeba. Mtu mmoja alisubiria kukaguliwa kwa muda wa dakika 15. Watu wengi walikuwa wakikosa usafiri kutokana na kukosa vigezo vya kuondoka nchini Uganda, huku wengine wakitiliwa shaka.

Kwa jinsi askari hao wa mpakani walivyokuwa makini katika ukaguzi wao, mimi niliamini kuwa safari yangu inaweza kuishia hapo. Wanaweza pia wakafanikiwa kugundua jeraha la risasi ambalo lilikuwa bado halijapona kabisa.

Tukiwa pembeni na yule mzee tuliendelea kujadili nini cha kufanya. Hadi kufikia muda huo tayari mzee alishakuwa ametumia kiasi cha shilingi 7,000 kuweza kufanikisha hadi mimi kufika kituoni hapo.

Hakuna mtu aliyegundua kuwa mimi nilikuwa ni kijana wa kiume. Kila aliyekuwa akipita karibu yangu, alijua kuwa mimi ni mwanamke tena mwenye umri wa zaidi ya miaka 60. Nilikuwa makini kuufunika uso wangu ili askari wasipate kunigundua.

Mzee alinipa shilingi 2,050 kwa ajili ya kutumia njiani, pesa iliyokuwa nyingi kupita uwezo wake wa kimaishia. Nilimtazama sana nishindwe kumtafakari.

Basi la kuelekea Kaisavuna lilikuwa limebakiza muda mfupi wa kuianza safari. Na ndilo lilikuwa basi pekee la kuelekea huko. Hivyo kama ningechelewa katika ukaguzi ambao nilikuwa na mashaka nao, basi niliona kwa siku hiyo nitakuwa nimekwama kuondoka Uganda.

Nilishangaa kuona mzee amekwenda hadi pale kwa askari na kumwita askari mmoja ambaye alikuja naye hadi pale nilipo.

“Unasemaje mzee, naona umeniitia pembeni. Unataka kunipa rushwa?” Aliuliza askari huyo aliyekuwa na bunduki begani.

“Samahani sana mkuu, huyu ni shemeji yangu anaumwa sana. Inatakiwa awahi kwenda kwa mwanaye. Naomba msaada wako apite pale bila kukaguliwa kwani akikaguliwa atachelewa na kama unavyoona basi la kwenda Kaisavuna limebaki moja tu na linakaribia kuondoka,” aliongea mzee huku akimpa pesa yule askari.

Askari alizitazama pesa zile, akanitazama na mimi niliyekuwa nikihema kwa siri na kwa woga mkubwa. Akarudi kumtazama mzee na kisha akasema. “Haya twende!” Sikuamini kama askari alikuwa amekubali, mashaka na hofu bado vilizidi kunitesa. Kwani nilijua huenda anaweza akubali lakini akifika eneo la ukaguzi awaamuru wenzake wanifanyie uchunguzi.

Nilimwaga mzee kwa hofu na kumshukuru kwa siri. Sikutaka kuongea, maana askari angenigundua kuwa mimi sikuwa mwanamke bali ni mwanamume. Alinifikisha hadi pale kwenye eneo la ukaguzi ambako kulikuwa na askari wengi wenye bunduki huku raia wengi waliokatazwa kusafiri wakiwa wamekalishwa chini.

“Jamani mwanamke huyu anaumwa na anawahi basi la Kaisavuna, naomba apite haraka tafadhali,” aliongea askari huyo aliyekuwa amechukua rushwa kutoka kwa mzee aliyekuwa amenisaidia.

Mungu ni mkubwa, askari waliniruhusu kupita. Upesi niliingia kwenye basi na kulipia haraka tiketi ya safari. Nikiwa ndani nilimtazama mzee aliyekuwa nje na kwa mbali. Machozi yalinitoka baada ya kumwona akitabasamu. Nilishindwa kumshukuru kwa kila hali maana eneo lile lilikuwa si la kujiachia sana.

Nilimpungia mkono wa kwa kheri naye akinipungia. Baada ya dakika 15 basi lilianza kuondoka kituoni hapo bado iliniwia vigumu kuamini kama naondoka kwenye ardhi ya Uganda.

Nilihisi safari yangu inaweza ikakwamia njiani na nikarudishwa tena kwenye mikono ya dikteta Idi Amini. Nilimwogopa sana mtawala yule. Moyo wangu uliendelea kunidunda ovyo, huku nikihema kwa mbali. Harufu ya kifo bado ilikuwa ikiishi ndani yangu sikuelewa ni kwanini.

Basi lilikiacha kituo cha Vumako na kuingia kwenye barabara ya kuelekea eneo la mpaka wa Kaisavuna na Uganda. Niliendelea kumwomba Mungu japo bado nafsi yangu iliendelea kutishwa na umauti.

Niliukumbuka msemo wa yule mzee aliokuwa ameniambia mara mbili na kwa nyakati tofauti kuwa, mimi ni mtu niliyekufa ambaye bado ninaishi. Msemo niliokuwa siuelewi.

Lakini mara zote nilizidi kujiuliza, imekuwaje hadi kufikia muda huo, bado nilikuwa nikipumua. Matukio mabaya yaliyonikuta nikiwa mbele ya kikosi cha jeshi cha mtawala Idi Amini, yalizidi kunipa wakati mgumu wa kuamini kuwa nilikuwa natoka salama ndani ya Uganda.

Nilijiuliza ndio yule mimi niliyekuwa nimevalishwa kitanzi nikitakiwa kunyongwa ndani ya kile chumba cha kutisha, chumba ambacho wenzangu sita raia wa nchi yangu walikuwa wamenyongwa? Sikudhani hivyo hata kidogo.

Mara moja nilijiuliza au mimi nilikuwa ni mzimu na sasa sijijui. Tukio ambalo lilinifanya nijiulize hivyo, lilikuwa ni lile tukio kuu la kutumbukizwa kwenye pipa la maji, ambalo nafsi yangu ilishakuwa imekiri kuwa mimi nilikuwa nimekufa.

Baada ya nusu saa basi lilifika katika mpaka wa Kaisavuna na Uganda. Kama kawaida wanajeshi wa Uganda walikuwa wakifanya ukaguzi. Bahati nzuri siku hiyo walikuwa kwenye ukaguzi maalumu wa malori yaliyokuwa yakitoka na kuingia Uganda.

Hivyo ukaguzi wa mabasi ulikuwa sio wa makini sana. Askari mmoja aliingia kwenye basi letu akatembea kuanzia mwanzo wa basi hadi mwisho akitutazama. Alipofika kwangu alinitazama sana kiasi cha kuibua hofu na jasho jembamba.

Aligeuka na kunipuuza, alishuka kwenye gari na kuruhusu basi kuingia nchini Kaisavuna.

Roho yangu ilishuka nilihema kwa nguvu, sikuamini kama nilikuwa naiacha Uganda. Nilichungulia dirishani na kutazama nyuma mara nyingi sana, hakika nilihisi furaha isiyoelezeka. Machozi mengi yalinitoka abiria waliokaa karibu yangu waliiona furaha yangu.

Nilianza kuinusa hali ya hewa ya nchi yangu ya amani. Sikuamini kama nakwenda kuonana na familia yangu tena. Ulikuwa unatimia mwezi wa tatu tokea nilipoondoka Kaisavuna kwenda Uganda. Sasa nilikuwa narudi nikiwa mwenye furaha.

Hata hivyo, bado nilikuwa nikijiuliza kifo changu kilikuwa kimekwenda wapi maana nilishakuwa nimejihesabia kuwa mimi ni marehemu. Nilijiambia mwenyewe kuwa huenda mimi nilikuwa nimefufuka kutoka katika kifo.

Maana kwa mara ya mwisho nilikuwa nimezinduka nikiwa miongoni mwa wafu. Kufumbua macho nikiwa juu ya maiti, maiti ambazo zilitakiwa kuchomwa moto, kulinifanya niamini kuwa mimi nilikuwa nimekwisha kufa na sasa nimefufuka.

Akili yangu ilianza kumfikiria mke wangu Paulina, mwanamke mrembo aliyekuwa ameiteka akili yangu na maisha yangu yote. Mtu aliyesababisha mimi nijitose kuingia ikulu ya Idi Amini na kuipeleleza Serikali yake.

Sasa nilijua kuwa nakwenda kuishi maisha mazuri pamoja na mke wangu nikiwa tajiri.

Kwa muda huo sikuwa tena na hofu juu ya ugumu wa maisha, kwani tayari nilishakuwa mtu tajiri kutokana na Serikali kuniwezesha kwa kila kitu kabla ya kuondoka kwenda Uganda na baada ya kuondoka. Kiasi kingine kikubwa cha pesa nilichokuwa nimeingiziwa benki, pindi nilipokuwa Uganda, kilinipa jeuri ya kujiona mimi ni tajiri wa maisha.

Nilimkumbuka mama yangu na kupanga kwenda kumwomba msamaha na hilo ndilo lilikuwa jambo muhimu na la kwanza. Nilitamani kwenda kushuka chini ya miguu yake na kulia mbele zake. Nilitamani kumwona dada yangu na watoto wake pamoja na mdogo wangu Zuni ambaye nilikuwa najua kwa miezi mitatu niliyokuwa nchini Uganda atakuwa amemaliza kidato cha tatu na sasa anaingia cha nne.

Mahaba mazito na utundu wa kitandani wa Paulina niliokuwa nimeukumbuka kwa zaidi muda wote huo, sasa niliamini nakwenda kuupata tena siku zote.

Safari iliendelea tukiwa tunakaribia Jimbo la Baikakulu. Niliamua kuvua ushungi kichwani na khanga iliyokuwa begani mwangu, kwa kuwa tayari nilikuwa nchini kwangu nikiwa huru kabisa. Abiria aliyekuwa kando yangu alianza kucheka baada ya kuona kidume nimevaa mavazi ya kike.

Nilitabasamu ikiwa ni siri yangu, pia abiria wote walinishangaa. Tulipofika Bakikulu basi lililala hapo. Nilikula chakula kizuri, nikanunua mavazi ya kiume na kuyavaa.

Siku ya pili yake saa 12 basi liliendelea na safari hadi likaupita mji wa Bidoa. Na baada ya saa saba, tulikuwa tunakaribia kuingia mji mkuu wa Kaisavuna Wimbodone, mji uliokuwa na kila aina ya watu na kazi. Furaha yangu ilikuwa kubwa sana sikuamini kama mimi Fredy Olutui nimerudi nyumbani.

Baada ya saa nne nyingine, basi lilifika mjini Wimbodone. Nilishuka na kwenda kwenye kituo cha mabasi ya kwenda kwenye mitaa ya mji, mabasi ya dakatwende. Nilipokuwa ndani ya basi tabasamu halikuondoka kwangu, furaha ilizidi kwa jinsi nilivyokuwa nikiiona mitaa mbalimbali.

Nilishuka mtaa wa Lego na kuelekea moja kwa moja nyumbani kwa mama yangu kwani nilikuwa nina hamu sana ya kumwona mama, dada zangu na mdogo wangu. Jambo kuu lilikuwa ni kuanguka chini ya miguu ya mama ili kumwomba msamaha na kumlilia kutokana na mambo ya kutisha yaliyokuwa yamenikuta nikiwa Uganda.

Nini kitaendelea? Usikose kesho.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.