MBAYA WA OKWI AMCHAGUA AJIB

Bingwa - - MBELE - NA MARTIN MAZUGWA

WASHINDWE wenyewe. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya mkali wa kupasia nyavu wa Tanzania Prisons, Mohamed Rashid, kusema kuwa anatamani siku moja kukitumikia kikosi cha Yanga chenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani.

Kauli ya straika huyo inamaanisha kwamba anatamani kucheza timu moja na Ibrahim Ajib, ambaye kwa sasa ni kama injini ya timu hiyo baada ya akina Donald Ngoma na mwenzake Amis Tambwe, kuonekana msimu huu hawako vizuri.

Rashid ni mbaya wa Okwi kutokana na ukweli kwamba, anayo mabao sita nyuma ya Mganda huyo anayeongoza akiwa na mabao nane, ambapo kati ya wawili hao mmoja akiteleza anaweza kutimuliwa vumbi.

Uwezo wa straika huyo umewaacha vinywa wazi wadau wa soka kutokana na upinzani mkubwa anaouonyesha kwa Okwi, jambo linalozifanya timu hizi kubwa za Simba na Yanga kuanza kummezea mate.

Akizungumza na BINGWA jana, Rashid alisema lengo lake ni kucheza soka katika klabu kubwa hapa nchini ikiwamo Yanga, ili aweze kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa ambapo mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wataiwakilisha nchi Ligi ya Mabingwa Afrika, mwakani.

“Hakuna asiyependa kucheza katika klabu kubwa kama Yanga, najua kwamba wapo wachezaji wazuri lakini naamini ninaweza kupambana mpaka nipate namba, napenda timu hizi ambazo zinashiriki michuano ya kimataifa,” alisema.

Straika huyo ni moja ya wale wanaotajwa kutakiwa na timu ya Yanga na yeye mwenyewe ameweka wazi kwamba licha ya kubakiza mkataba wa mwaka mmoja, anaweza kuondoka endapo Yanga watazungumza na Prisons na kumalizana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.