MADAKTARI WAZIPA SOMO TIMU ZINAZOUOTA UBINGWA VPL

Bingwa - - TANGAZO - HUSSEN OMAR NA ZAINAB IDDY

WAKATI ushindani ukizidi kuongezeka kwa timu shiriki kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, madaktari wamezishauri kuhakikisha wachezaji wao wanaopata majeraha wanafuata ushauri waliopewa ili kuvisaidia vikosi vyao kufanya vema ikiwezekana kutwaa ubingwa.

Ingawa ni mapema kutabiri atakuwa nani, lakini hadi sasa klabu zinazoonekana kuwa kwenye ushindani wa kuwania taji msimu huu ni Simba, Azam FC, Yanga, Mtibwa na Singida United.

Wakizungumza na BINGWA kwa nyakati tofauti, madaktari hao waliokuwapo katika Chama cha Wataalamu wa Tiba za Michezo Tanzania (TASMA), walisema yapo magonjwa na majeraha mengi yanayoweza kumweka nje kwa muda mrefu mchezaji au kutoweza kurudi kabisa uwanjani.

Katibu Mkuu wa TASMA, Nassoro Matuzya, alisema sababu nyingine inayokwamisha wachezaji wanaokuwa na majeraha ya goti kuchukua muda mrefu kupona ni umri, kukosa matunzo na kutumika muda mrefu bila ya kupumzika.

“Unajua haya majeraha ya wachezaji kupona kwake haraka au taratibu pia inategemea na umri wa mchezaji, matunzo anayoyapata, lakini pia kutumika kwa muda mrefu kunachangia kuchelewesha uponaji wa majeraha hayo,” alisema Matuzya.

Kwa upande wa daktari wa kikosi cha Taifa Stars, Richard Yomba, alisema: “Maradhi yoyote yatakayopatikana kwa mchezaji na kutoweza kutibiwa kwa usahihi au kufuata masharti yanaweza kumletea madhara mchezaji, hivyo ni lazima wawe makini katika kazi yao na hata matibabu wanayopewa wanapoumia.

“Mfano mzuri ni magonjwa kama ‘hernia’, pulmonary embolism (donge la damu kuziba mishipa ya damu katika mapafu), goti, kifundo cha mguu (enka) na nyonga.

“Mengine hapo unaweza kuyaona madogo, lakini usipopata tiba sahihi yanaweza yakakuletea madhara makubwa na hata kusitisha safari ya mchezaji kisoka,” alisema.

Alishauri timu kujenga utamaduni wa kuwapima wachezaji wao kabla ya kusajili ili kuwaepusha kutumia fedha nyingi kunasa wachezaji ambao mwisho wa siku, wataishia benchi kutokana na kukabiliwa na majeraha.

Yanga ni miongoni mwa timu za Ligi Kuu Bara ambayo wimbi la majeruhi linaloelekea kuathiri kampeni yao ya kutetea ubingwa wao, kwani wachezaji wake tegemeo, Thaban Kamusoko, Amis Tambwe, Donald Ngoma na Benno Kakolanya; wote wapo nje ya uwanja kutokana na kukabiliwa na majeraha ya muda mrefu.@@

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.