Ndanda kusajili fowadi wawili wakali

Bingwa - - TANGAZO - NA SALMA MPELI

NDANDA wamepanga kusajili fowadi wawili katika usajili wa dirisha dogo linalotarajiwa kufunguliwa Novemba 15, mwaka huu.

Wakizungumza na BINGWA jana Kocha Mkuu wa Ndanda, Malale Hamsini, alisema anahitaji kufanya marekebisho kidogo hasa kwenye nafasi ya ushambuliaji.

Hamsini alisema hahitaji marekebisho makubwa katika kikosi chake, bali ataongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ili waweze kupata ushindi kwenye michezo yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha huyo alisema atasajili washambuliaji hao baada ya kuona kuna mapungufu katika idara hiyo kutokana na michezo tisa ya mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.

Alisema tayari amewaona wachezaji wanaokidhi viwango vya kuwasajili katika kikosi chake, lakini hawezi kuweka wazi majina yao kwa kuhofia kufanyiwa hujuma na timu nyingine.

Hamsini alisema anatarajia kukabidhi ripoti yake kwa uongozi wa klabu hiyo, baada ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ruvu Shooting.

“Ndanda ipo vizuri na inahitaji marekebisho kidogo sana,” alisema Hamsini.

Katika hatua nyingine, kocha wa Njombe Mji, Mrage Kabange, alisema atafanya maboresho katika safu ya ushambuliaji, baada ya kuona kuna tatizo kubwa katika kupata ushindi.

“Ripoti ipo tayari na tutaikabidhi wakati wowote kuanzia sasa, lakini marekebisho yatalenga zaidi kwenye safu ya ushambuliaji ambayo inaonekana tatizo,” alisema Kabange.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.